The House of Favourite Newspapers

MZIMU WA KANUMBA WAMTOKEA MTOTO KONGO

WANANDOA kutoka Jamhuri ya Kidemo-krasia ya Kongo, Numbi Mwilambwe (35) na mkewe Ngoy Mfumuabana (30), wameeleza namna mtoto wao mdogo, Felix alivyotokewa na kuteswa na mzimu wa aliyekuwa mwigizaji kinara wa Bongo Movies, marehemu Steven Kanumba, Risasi Mchanganyiko lina mkasa mzima.

Familia hiyo ilizua kizaazaa mwishoni mwa wiki iliyopita nyumbani kwa mama Kanumba, Flora Mtegoa maeneo ya Kimara-Temboni jijini Dar ambapo Wakongo hao waligoma kuondoka nje ya geti la mama huyo baada ya kufunga safari na kutinga Bongo. Mashuhuda waliliambia Risasi Mchanganyiko kuwa, wanandoa hao na watoto wao watatu walijikuta wakilala nje ya nyumba ya mama Kanumba baada ya kumkosa kwa maelezo kuwa yupo mkoani.

Pamoja na majirani kuwaeleza kuwa mama Kanumba hayupo, waliendelea kung’ang’ania kukaa getini hapo hadi pale mama huyo atakaporejea ili wapate idhini ya kumpa mtoto wao jina la Kanumba ikiwa ni masharti mazito aliyopewa mama wa mtoto huyo na Kanumba ndotoni. Wanandoa hao waliwaeleza majirani wa mama Kanumba kuwa, endapo hawatampa mtoto wao Felix jina la Kanumba atakuwa anaumwa, jambo ambalo limekuwa likiwatesa yapata miezi sita sasa.

SIMULIZI

Katika mahojiano na Risasi Mchanganyiko, Numbi alisema kuwa, mkewe ndiye aliyeanza kumuota Kanumba, lakini yeye alikuwa akimbishia kila siku na kumuona muongo. Alisema kuwa, alikuwa akimuona mkewe muongo kwa sababu alishawahi kusikia kuwa msanii huyo ambaye alikuwa anaishi Tanzania alishafariki dunia sasa iweje mkewe amuote?

Lakini alisema kuwa, baada ya muda fulani, yeye mwenyewe (Numbi) alianza kumuota kwamba, asipomuita mwanaye (Felix) jina la Kanumba, basi mtoto huyo atakufa.Alisema awali hakuamini mara moja, aliamua kuipuuzia ndoto hiyo kwa sababu yeye ni mchungaji, lakini baada ya muda mtoto wao alianza kuumwa.

“Kilichotuleta sisi huku Dar es Salaam ni kuja kuonana na mama Kanumba kama ambavyo Kanumba katuagiza ndotoni. “Sisi hatuna ndugu huku Dar na wala hatukuwahi kuonana na Kanumba enzi za uhai wake, ila imetulazimu kuja kwa sababu baada ya mke wangu kujifungua mtoto wetu huyu wa mwisho, tukaamua kumuita Felix, lakini mke wangu alianza kumuota Kanumba akimuambia kuwa tumuite mtoto wetu jina lake.

“Hatukufanya kama ndoto ya mke wangu ilivyotaka ndipo mtoto alipoanza kuumwa, tukampeleka hospitalini, lakini hakupona. “Mke wangu alimuota tena Kanumba akimwambia msipomuita mtoto jina la Kanumba, mtoto atakufa.

“Bado mimi sikuamini kwa sababu mimi ni mchungaji, tukaendelea na maisha, lakini mtoto akaanza kuvimba sehemu za siri, ikabidi tumrudishe hospitalini, lakini haikusaidia. “Mke wangu aliendelea kuota kuwa tuache kumpa dawa na asubuhi ule uvimbe haukuwepo tena.

“Baada ya hapo na mimi nikaota Kanumba amekuja hivi kabisa, akaniambia kama ninataka mtoto apone, ni lazima tumwite jina lake. “Hapo ndipo tulipokubaliana naye, tukaanza kumuita Kanumba, akaacha kuumwa kabisa.

“Mimi nikamuota ananiambia tumpeleke mtoto Tanzania kwa mama yake (mama Kanumba) ili akamuone na ampe idhini ya kutumia jina hilo kwa mtoto wake, sasa nikawa ninawaza tutaendaje Tanzania na hatuna ndugu? Tutafikia wapi? Tutaishi vipi? Akawa anaendelea kutusumbua.

“Ilibidi mimi na mke wangu tuuze mkaa ili tupate pesa ya kuja Tanzania. Tulipopata nauli ndiyo hivi tumefika ila pesa zote tuliibiwa tukiwa Zambia.

“Tulipofika Dar, tulimuomba dereva teksi atupeleke nyumbani kwa mama Kanumba ndipo akatuleta, lakini tumeambiwa amesafiri yupo Dodoma. “Baada ya kuzuiwa kuingia ndani, tumelala hapa nje hadi tukaishia mikononi mwa Serikali ya Mtaa wa Upendo, Kimara-Temboni baada ya kupelekwa kwa Balozi wa Nyumba Kumi,” alisimulia Numbi.

MWENYEKITI WA MTAA

Gazeti hili lilizungumza na Mwenyekiti wa Mtaa wa Upendo, Agwelino Kalinga ili kujua kama ana taarifa za watu hao, Raia wa Kongo ambapo alifunguka;

“Nimepata taarifa kuwa kwa Mjumbe wa Shina Namba Tatu kuna wageni ambao wamejitambulisha kuwa wametoka Kongo na wamekuja kwa mama Kanumba, wanadai wameoteshwa kwamba mtoto wao wa mwisho aitwe Kanumba na wafike huku, wawasiliane na mama Kanumba ili atoe idhini ya wao kutumia jina hilo, sijaamini sana hivyo vitu vya kuoteshwa, lakini kuwasikiliza ni muhimu japokuwa ni mambo ya kiimani zaidi.

“Mama Kanumba mwenyewe nilipompigia simu alisema hawatambui watu hao na hataki wageni kwake ndiyo ikabidi tuwahifadhi hapa kwa mjumbe ili taratibu zifuatwe ikiwemo kuangalia kama vibali vyao vinawaruhusu kuwepo hapa na kama havina hitilafu au udanganyifu wowote,” alisema Agwelino Kalinga.

MAMA KANUMBA SASA

Akizungumza na gazeti hili juu ya suala hilo, mama Kanumba alisema yeye anachotaka asiwakute nyumbani kwake kwani watu hao hawafahamu. “Kama wanataka jina watumie tu wala mimi sina tatizo. Kwa nini asinioteshe mimi mama yake awaoteshe wao? Wao kama akina nani? Mimi sikubaliani nao. Kama wao wameota, mimi sijaota, kwa hiyo mimi sina uhakika kama kweli wameota au hawakuota na Kanumba ni jina tu.

“Wakitaka wamuite maana ni jina tu kama majina mengine, halinunuliwi dukani, ni kama ukisema Flora au Steven ila jina kama jina waendelee tu kumuita mimi wala sina tatizo.

WAFURAHI

Baada ya kusikia kauli hiyo kutoka kwa mama Kanumba watumie jina hilo walifurahi mno na kuomba kusaidiwa kurudi kwao Kongo kutokana na wao kukosa pesa ya kurudi kwa sababu waliibiwa wakiwa Zambia.

HADI POLISI

Katika hali kama hiyo, watu hao walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Mbezi- Kwayusuf ili watafutiwe utaratibu wa kurejeshwa nchini kwao.

STORI: Shamuma Awadhi,Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.