The House of Favourite Newspapers
gunners X

Papa Francis Afichua Jinsi Alivyonusurika Kuuawa Kwenye Ziara Yake Nchini Iraq

0

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amefichua jinsi alivyonusurika kuuawa katika mtego aliokuwa ameandaliwa jijini Baghdad, Iraq alipofanya ziara Machi, 2021.

Katika kitabu chake anachotarajia kukichapisha hivi karibuni, Papa Francis ameeleza kuwa tukio hilo lililotokea wakati wa ziara yake nchini Iraq ambapo taarifa za kijasusi kutoka Uingereza, zilieleza kuwa eneo analotarajiwa kwenda kuhutubia, kulikuwa na walipuaji wawili wa kujitoa mhanga waliokuwa wakimsubiri ili walipue mabomu na kumuua.

“Washambuliaji wote wawili walikamatwa na kuuawa na ziara yake ilifanyika kwa siku tatu,” amenukuliwa Papa Francis katika sehemu zilizochapishwa na Gazeti la Italia, Corriere della Sera.

Ziara hiyo iliyofanyika kwa siku tatu wakati wa Janga la Virusi vya Corona, ilikuwa ziara ya kwanza kabisa kwa Iraq na Papa na ilifanyika chini ya ulinzi mkali.

Miaka kadhaa iliyopita, kulishuhudiwa ongezeko la vurugu za kimadhehebu nchini Iraq, na mapigano kati ya Waislamu wa Shia na Sunni pamoja na mateso ya wachache wa kidini.

Jumuiya ya Wakristo nchini humo ilipungua kwa kiasi kikubwa, baada ya kulengwa hasa na kundi la Islamic State na wanamgambo wa Sunni wenye msimamo mkali.

Katika sehemu za wasifu wake, Papa anasema: “Karibu kila mtu alinishauri nisifanye ziara hiyo lakini nilihisi napaswa kuifanya,” alisema.

Anasema mpango huo uligunduliwa na maafisa wa ujasusi wa Uingereza, ambao waliwatonya polisi wa Iraq, nao wakamwambia Papa na timu yake ya usalama mara tu alipowasili.

Kitabu hicho, kinachoitwa Tumaini, kinatarajiwa kuchapishwa Januari 14, 2025.

Vatican haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni, kulingana na Shirika la Habari la Reuters.

Leave A Reply