The House of Favourite Newspapers
gunners X

Polisi Ashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya raia, vifo vitatu vyachunguzwa

0

Jeshi la Polisi Tanzania linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na matukio matatu tofauti ya vifo yaliyotokea katika maeneo ya Tarime/Rorya, Jijini Arusha na Wilaya ya Rufiji kwa nyakati tofauti.

Tukio la Kwanza – Tarime/Rorya

Tukio la kwanza linahusu kifo cha Dickson Tadeus Joseph, mkazi wa Rebu Senta, Wilaya ya Tarime, kilichotokea tarehe 01 Januari 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi limepokea barua ya malalamiko ikidai kuwa kifo hicho hakikusababishwa na marehemu kuanguka katika Mtaa wa Serengeti alipokuwa akikimbia, kama ilivyotangazwa awali, bali kinadaiwa kusababishwa na askari Polisi.

Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa kina, na endapo ushahidi kutoka kwa mashuhuda utabaini kuwa askari alihusika, hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Tukio la Pili – Jijini Arusha

Tukio la pili linahusu kifo cha Viollete Uwumuhoza, raia wa Rwanda, aliyefariki tarehe 07 Januari 2026 baada ya kujinyonga akiwa mahabusu katika kituo cha Polisi Jijini Arusha.

Marehemu alikuwa akishikiliwa kwa kosa la kuingia na kuishi nchini kinyume cha sheria. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa haraka na wa kisayansi ili kubaini mazingira kamili ya tukio hilo.

Tukio la Tatu – Rufiji

Sambamba na matukio hayo, Jeshi la Polisi linamshikilia askari mmoja wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji kwa tuhuma za kumpiga risasi Shaban Said Luluba, mkazi wa Kijiji cha Nyamwage, Wilaya ya Rufiji, tukio lililotokea leo tarehe 08 Januari 2026 wakati wa utekelezaji wa ukamataji.

Uchunguzi unaendelea, na endapo itabainika kuwa kulikuwa na uzembe au matumizi ya nguvu kupita kiasi, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya askari huyo.

Jeshi la Polisi linasisitiza kuwa linaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote.

 

Leave A Reply