The House of Favourite Newspapers
gunners X

Polisi waanza uchunguzi wa picha ya raia wa kigeni na mifuko ya fedha

0
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime

Jeshi la Polisi Tanzania limethibitisha kuanza uchunguzi wa kina kufuatia kusambaa kwa picha mjongeo inayomwonesha raia wa kigeni mwenye asili ya China akiwa na mifuko ya sandarusi iliyojaa fedha taslimu, zikiwemo fedha za ndani na za kigeni, tukio lililozua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii.

Akizungumza na gazeti la Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema uchunguzi tayari umeanza na kwamba taarifa kamili itatolewa baada ya hatua za uchunguzi kukamilika ili kubaini ukweli wa tukio hilo na chanzo cha fedha hizo.

“Nilikuwa kwenye kikao, nimetoka ndipo nimeiona hiyo picha mjongeo. Uchunguzi umeanza na tunaifuatilia ili kupata taarifa kamili kisha kuitoa kwa vyombo vya habari kueleza tukio hilo,” amesema Misime.

Picha mjongeo hiyo, iliyosambaa jana, inamuonesha raia huyo wa kigeni akiwa amezungukwa na watu wanaodhaniwa kuwa maafisa wa usalama waliovaa kiraia, wakimpa maelekezo ya kuzitoa fedha hizo kutoka kwenye mifuko mitatu ya sandarusi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, tukio hilo linadaiwa kutokea nyumbani kwake katika eneo la Oysterbay, Mtaa wa Mazengo, nyumba za Phoenix, jijini Dar es Salaam.

Taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zinaeleza kuwa majirani pamoja na viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Oysterbay walitoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama, hatua iliyopelekea kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

Aidha, taarifa hizo zinaeleza kuwa raia huyo wa kigeni akiwa na wenzake walikuwa wakitoka nyumbani kwao majira ya saa 1:30 usiku na kurejea saa 10:00 alfajiri, wakiwa na mifuko iliyojaa fedha, jambo lililozua mashaka miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya kukamatwa, watuhumiwa walikutwa na fedha taslimu zikiwemo Dola za Marekani na Shilingi za Tanzania, zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni sita, fedha ambazo ziliripotiwa kufichwa ndani ya nyumba namba 317, ghorofa ya tatu.

Jeshi la Polisi halijathibitisha rasmi kiasi hicho cha fedha wala uhalali wake, likisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea kabla ya kutoa tamko la mwisho kwa umma.

Leave A Reply