The House of Favourite Newspapers
gunners X

Raia Wawili wa China Wakabiliwa na Kesi ya Uhujumu Uchumi – Video

0

Raia wawili wa China, Weisi Wang (41) na Yao Licong, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwemo kosa la utakatishaji fedha zenye thamani ya takribani Shilingi Bilioni Mbili na Milioni Kumi na Tatu za Kitanzania.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na Mawakili wa Serikali Wakuu, Patrick Mwita na Benjamin Muroto, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo, washtakiwa wote wanakabiliwa na shtaka la kuongoza genge la uhalifu, wakidaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Desemba 1, 2024 na Desemba 30, 2025, katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza na Unguja Zanzibar, pamoja na maeneo mengine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Inadaiwa kuwa washtakiwa walikusudia, kuandaa na kuongoza genge la uhalifu lililojihusisha na kughushi nyaraka, kunakili kadi za ATM, kukwepa kodi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la pili, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa la utakatishaji fedha, ambapo inadaiwa walimiliki Dola za Kimarekani 707,075 pamoja na Shilingi za Kitanzania 281,710,000, wakijua kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu wa kuongoza genge la uhalifu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Beda Nyaki amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Aidha, mahakama imeeleza kuwa kutokana na uzito wa mashtaka yanayowakabili, washtakiwa hawa hawana sifa ya kupata dhamana katika ngazi ya mahakama hiyo.

Upande wa Jamhuri umeeleza kuwa upelelezi wa shauri bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa, ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 21, 2026.

Leave A Reply