Rais Mwinyi Azuia Vikao Kufanyika Hoteli za Kitalii, Aagiza Udhibiti wa Matumizi ya Serikali

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameagiza makatibu wakuu wa wizara kusitisha mara moja tabia ya kuidhinisha vikao na mikutano ya kiserikali kufanyika katika hoteli za kitalii.
Agizo hilo limetolewa Novemba 22, wakati wa hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali huko Unguja.
Dk. Mwinyi alisema hatua hiyo inalenga kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ndani ya serikali, na kuelekeza viongozi hao kuhakikisha kuwa mapato yanaongezeka huku matumizi yakidhibitiwa kikamilifu.
Amesisitiza kuwa matumizi ya rasilimali za umma lazima yawe ya busara, yenye tija na yanayoendana na malengo ya serikali ya kubana matumizi na kuongeza ufanisi.


