The House of Favourite Newspapers

Rais Samia awezesha mageuzi Makubwa Ocean Road

0

 

…..Madaktari wake waenda Comoro kutoa tiba

…..Wamo pia wa JKCI, MOI, Muhimbili na Benjamin Mkapa

MADAKTARI bingwa wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ni miongoni mwa ujumbe wa watu 53 ambao tayari wametua nchini Comoro kwaajili ya kambi ya wiki moja ya matibabu.

Wataalamu hao waliondoka nchini jana kwa ndege ya Shirika la Precision Air kwaajili ya kambi hiyo inayotarajiwa kuanza kesho Jumapili nchini humo.

Dk Diwani Msemo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, na daktari bobezi wa magonjwa ya saratani alisema Ocean Road ni taasisi ambayo imekuwa kinara kwa matibabu ya saratani kusini mwa jangwa la sahara

“Ukiondoa Afrika Kusini, Ocean Road ndiyo hospitali bora kuliko zote kwenye ukanda huu na haya yote yasingewezeka kama siyo uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka minne iliyopita amewekeza shilingi bilioni 40 kwenye miundombinu, vifaa vya kisasa na kusomesha madaktari bingwa,” alisema.

Alisema hospitali hiyo imefanikiwa kutoa huduma za afya za mkoba kwa kuzunguka kwenye mikoa mbalimbali nchini kutibu wagonjwa wa saratani ambao wasingeweza kwenda Ocean Road.

“Sasa tunakwenda nje ya Tanzania kuwapa huduma ya saratani na tumebaini kuwa Comoro hawana huduma kama hizo wanategemea nchi za India na uarabuni kwa hiyo kwetu ni fursa kuwapa huduma za kibingwa kwa gharama nafuu,” alisema

“Hapa Tanzania watazipata kwetu kwa gharama nafuu kulinganisha na kwingineko na huduma watakazokuja kuzipata hapa zitatuingizia fedha ambazo zitawasaidia watanzania wasio na uwezo wa kugharamia matibabu ya saratani,” alisema Dk. Msemo

“Nakwenda Comoro na timu ya madaktari bingwa na wauguzi tunakwenda kuwapima kule na kuwapa ushauri na watakaoonekana wanasaratani wataletwa Tanzania kwaajili ya matibabu zaidi na tunashukuru kwasababu haya yote ni maono ya Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema

Madaktari waliokwenda Comoroni kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma na maofisa wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD)

Mkurugenzi Mkuu wa JKCI ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Utalii Tiba, Dk Peter Kisenge alisema wanakwenda Comoro kutimiza ahadi iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa nchini humo mwaka huu wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wao.

“Madaktari waliokwenda Comoro Desemba mwaka jana Desemba walihudumia wananchi 2,700 na kati ya hao 271 walipata rufaa ya kuja Tanzania na walikuja hapa nchini tunashukuru sana mwitikio ulikuwa mkubwa na ndipo Rais wa Comoro alipomwomba Rais Samia turudi tena kule,” alisema

“Tunakwenda Comoro chini ya kitu tunaita tiba mkoba ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo tumezunguka mikoa mbalimbali nchini na sasa inavuka mipaka kwenda Comoro, Malawi, Congo na Burundi, nia ya kuvuka mipaka ni kuzieleza nchi zingine uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya awamu ya sita,’ alisema Dk Kisenge

Aidha, alisema serikali ya awamu ya sita imewekeza kwenye vifaa tiba na rasilimali watu kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba mataifa mengi yanakuja kujifunza mambo mbalimbali kuhusu tiba.

“Tumepeleka madaktari bingwa wabobezi, watu wa maabara, wauguzi tutatoa huduma ya matibabu ya aina mbalimbali na wapo wagonjwa watahitaji kuja kwa matibabu nchini Tanzania, watakaoletwa huku wataleta pesa za kigeni ambazo zitawanufaika watanzania kwa miradi ya maendeleo,” alisema

Alisema wanamikakati ya kwenda nchi mbalimbali kwa ajili ya kutoa tiba kama Afrika ya Kati, DRC Congo na visiwa vya Shelisheli na kwamba dhamira ya Rais Samia ni kuongeza diplomasia kupitia utalii tiba.

 

 

Leave A Reply