Rais Samia: Matukio ya Oktoba 29, Yalipangwa kwa Lengo la Kuangusha Dola – Video

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema matukio yaliyotokea kuanzia Oktoba 29, 2025 na kuendelea yalikuwa matukio ya kutengenezwa ambayo yalikuwa na lengo la kuangusha dola ya nchi yetu.
Ameyasema hayo leo Disemba 02, 2025 akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Dar Es Salaam katika ukumbi wa mikutano wa JNICC.
“Lililotokea ni tukio la kutengeneza na waliolipanga walidhamiria kuangusha dola ya nchi yetu”
Rais Samia ameeleza kuwa vijana walioshiriki matukio hayo walimezeshwa maneno ya kufanya kama ‘yaliyotokea Madagascar’ huku akieleza kuwa vijana hao ukiwahoji yaliyotokea Madagascar ni yapi hawajui. Rais Samia amesema wapo pia watu wasiokuwa na matatizo ya maisha wanaofadhili machafuko kwa maslahi yao binafsi, akiwataja kama “si Watanzania kamili kamili” kwa kuwa wana uwezo wa kujiondoa nchini wakati matatizo wanayochochea yakitokea.

Ameonya kuwa tofauti za kidini, kisiasa au kimtazamo zisigeuzwe chanzo cha kuvuruga amani ya Tanzania.
“Tusivurugwe ndugu zangu kupitia dini au siasa. Hatupaswi kuivuruga nchi yetu kwa sababu tu humpendi aliyepo serikalini,” amesisitiza.
Akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, Rais Samia amesema sio sahihi kuyaita makosa wakati yanawanufaisha Watanzania moja kwa moja.
“Kama kosa letu ni kueneza huduma bora za afya hadi vijijini, kujenga shule nzuri au kukuza uchumi—hilo si kosa. Kama humpendi anayeongoza, basi stahimiri tu. Hii ni nchi ya demokrasia,” amesema.


