Rais Wa Malawi Yuko Tanzania Kwa Ajili Ya Mkutano Wa Nishati Wa Afrika

Rais wa Jamhuri ya Malawi, Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera, amewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati unafanyika tarehe 27 na 28 Januari 2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.
Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dkt. Chakwera alilakiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Saada Mkuya, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Cosato Chumi na maafisa waandamizi wa serikali

Mkutano huo unawaleta pamoja Wakuu wa Nchi za Afrika, wataalam wa nishati, viongozi wa sekta binafsi, na washirika wa maendeleo kwa ajili ya kujadili mikakati ya kukabiliana na changamoto za nishati na kuchangamkia fursa za bara la Afrika. Moja ya matokeo muhimu ya mkutano huo ni kupitishwa kwa Azimio la Dar es Salaam, linalosisitiza dhamira ya pamoja ya viongozi wa Afrika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu kwa maendeleo ya bara hili.


