RUKWA: KITOWEO CHA PANYA CHAZUA BALAA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, akizungumza na wananchi.

 

RUKWA: Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amezua balaa kutokana na wananchi mkoani kwake kufanya panya kuwa kitoweo hivyo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Khalfan Haule kuhakikisha anatafuta dawa ya kuwaua wakiwa mashambani ili kuokoa miti kutokana na uchomaji wa misitu unaofanywa na watu wanaowatafuta wanyama hao.

 

Agizo hilo alilitoa hivi karibuni katika muendelezo wa kampeni ya upandaji miti mijini na vijijini katika Kijiji cha Mpwapwa, Kata ya Mpwapwa, wilayani Sumbawanga baada ya kuwauliza wananchi wa kijiji hicho juu ya changamoto aliyoisikia ya uchomaji wa moto misitu kutokana na kuwinda panya na wananchi kukataa.

 

Alisema kuwa ameisikia changamoto hiyo ya uchomaji wa misitu kwa sababu ya uwindaji wa panya kutoka kwa vijana mbalimbali wanaojishughulisha na mashamba ya upandaji miti pamoja na taarifa iliyosomwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga juu ya changamoto za kuendeleza misitu mkoani humo.

Picha ya maktaba.

“DC tafuta dawa ya panya, wauliwe huko mashambani, ili panya wasiwepo na miti iokoke, mbona hamshangilii? Hawa panya tutawaua kwa sumu huko mashambani wasiwe chanzo cha moto ambayo mnachoma huko kuwatafuta hawa panya ili wafie hukohuko mashimoni msiwapate,” alisisitiza huku baadhi ya wananchi walioonekana watumiaji wa kitoweo hicho wakisikitika.

Pia katika kuongezea hilo alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuhakikisha anasimamia sheria ya hifadhi ya mazingira na kuwawajibisha wote wanaohusika na uharibifu wa mazingira.

 

Akisoma risala, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Nyangi Msemakweli alishindilia kwa kubainisha kuwa miongoni mwa changamoto ni muitikio mdogo wa uhifadhi wa mazingira pamoja na mila na tamaduni za wananchi wake za uwindaji wa panya hali inayosababisha uchomaji wa misitu wakati wa kiangazi.

 

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Steven Sichula alilipokea kwa masikitiko agizo hilo la mkuu wa mkoa na kusema siyo haki kuwamaliza panya wote kwani nao ni viumbe hai, wanahitaji kuishi na ni kitoweo kwao ambacho kinawapa protini ambapo alishauri utafutwe utaratibu mwingine wa kukomesha tabia hiyo lakini siyo kuwaua panya wote.

 

Serikali mkoani Rukwa imesema inafanya mkakati wa kuwamaliza panya wote porini kwani wamekuwa ni sababu ya wakazi wa mkoa huo kuchoma moto misitu kwa nia ya kutafuta panya ili watumie kama kitoweo.

 

Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliishauri serikali kuelimisha jamii kabla ya kutumia sumu hiyo ya kuwaua panya hao ili wananchi waelewe kwamba wakifa hawatafaa kuliwa ili kuepusha madhara kwa binadamu.

Katika msimu wa mwaka 2017/2018 halmashauri ya Wilaya ya Sumbwanga imepanda miti 830,527 ambayo ni sawa na asilimia 55.4 na ina misitu 92 yenye ukubwa wa hekta 49,179.6.

 

STORI: MWANDISHI WETU, RUKWA

Toa comment