The House of Favourite Newspapers

Ruvuma: RC Aachunguza Kifo cha Mlinzi

0

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma (RC), Benson Mpesya

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma (RC), Benson Mpesya.

Stori: Stephano Mango, RISASI JUMAMOSI

Ruvuma: Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma (RC), Benson Mpesya ameunda kamati ya wajumbe 10 inayoongozwa na Mkuu wa Mafunzo ya Kivita wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Kanda ya Kusini ya Tembo, Brigedi Kanali Idd Said Nkambi kuchunguza tukio tata la mauaji linalohusisha Polisi wa Kituo Kikuu cha Mjini Songea mkoani hapa.

Mpesya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea alisema kuwa tukio la mauaji ya Massanja Aliyo (38) aliyekuwa mlinzi kwenye Machinjio ya Ng’ombe ya Manispaa ya Songea lilimlazimu kuunda kamati hiyo ambayo itafanya kazi kwa siku 14 kufuatia mkanganyiko wa taarifa juu ya kifo hicho kwa madai kwamba alipigwa na polisi.

Alisema kuwa kamati hiyo haitakuwa na mjumbe kutoka Jeshi la Polisi ili kubaini ukweli wa tukio zima huku akiwataka wananchi ambao wanafahamu ukweli kutoa ushirikiano kwenye kamati hiyo ili haki itendeke.

Kuhusu tukio hilo, ilielezwa kuwa, usiku wa Mei 8, mwaka huu, Massanja akiwa lindoni alidaiwa kuvamiwa na watu watatu waliovalia makoti marefu ya polisi kisha kumpiga na kumuacha akiwa mahututi na kukimbilia kusikojulikana.

Ilidaiwa kuwa muda mfupi, polisi walifika na kuukuta umati ukimshuhudia jamaa huyo akiwa mahututi ambapo walimchukua na kumkimbiza katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma ambako madaktari walithibitisha kifo chake huku lawama zikielekezwa kwa polisi.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, ACP Zuber Mwombeji alithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa madai kwamba alipigwa na watu wasiofahamika.

Leave A Reply