Samia: Serikali ya CCM Inafanya Kazi kwa Kuheshimu Utu wa Mtanzania
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Septemba 5, 2025, amesimama kuwasalimia na kuomba kura kwa maelfu ya wananchi wa Jimbo la Uyole, Mbeya, waliokuwa wamemiminika barabarani kumpokea.
Akizungumza na wananchi hao, Dkt. Samia amesema serikali ya CCM imejipanga kuendeleza jitihada za maendeleo kwa kuzingatia ustawi wa jamii, kupitia dira ya “Kazi na Utu Tunasonga Mbele.”
“Sisi tunasema kazi na utu. Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya kazi ikijua ina watu wa kuwatumikia na kuheshimu utu wa Mtanzania. Tunapambana kuhakikisha uchumi unakua, ustawi wa jamii unakuwepo, na maisha ya wananchi yanakuwa bora,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, alieleza kuwa haingekuwa sawa kuelekea Jimbo la Rungwe bila kusimama Uyole, ambalo ni jimbo la Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dkt. Tulia Akson.
Wananchi wa Uyole walimkaribisha kwa shangwe na vigelegele, wakionesha mshikamano na hamasa ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao.