Sholo Mwamba: Nitawapiga KO Makabila, Man Fongo

MKALI wa Muz-iki wa Singeli, Sholo Mwamba ameweka wazi kuwa atahakikisha anawakalisha mahasimu wake katika muziki huo mapema kabisa kwa KO kwenye shoo kubwa iliopewa jina usiku wa mwisho wa ubishi.
Mkali huyo ambaye ni miongoni mwa wasanii wa muziki huo watakaopanda kwenye jukwaa moja na wakali wengine ambao ni Man Fongo na Dulla Makabila katika pambano hilo litakalofanyika Aprili Mosi, mwaka huu (Sikukuu ya Pasaka) kwenye Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem, Dar.
Akizungumza na Risasi Vibes, Sholo Mwamba alisema siku zote amekuwa juu katika matamasha mbalimbali kwa kuwa yeye ni mwamvuli wa wengine kwenye muziki huo hivyo lazima atawakalisha wapinzani wake.
“Ukiangalia katika huu mpambano unaona kabisa jina langu lipo juu ya wengine sasa hapo utaona kwa nini imekuwa hivyo kwa sababu mimi ni kama mwalimu wao na wao ni wanafunzi wangu, sasa wanafunzi wanapambana kwa ajili ya kutaka kumpita mwalimu ila siku zote tunasema mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu.
“Naomba mashabiki wangu waje kwa wingi siku hiyo kwani yaliopita yamepita kwa sababu nina uhakika hawa niliopangwa nao katika kazi hii hawatoweza kutoka maana nataka niwapige KO ya mapema pale Dar Live siku hiyo,” alisema Sholo Mwamba.
Kwa upande wa mratibu wa shoo hiyo na meneja wa Dar Live, Rajab Mteta ‘KP Mjomba’ alisema mbali ya mchuano huo kutakuwa na vita nyingine ya wakali wa Taarabu kati ya Jahazi Modern na Yah TMK.
KP Mjomba aliongeza kuwa kiingilio katika shoo hiyo ya aina yake kitakuwa ni buku saba yaani shilingi 7,000 huku michezo mbalimbali ya watoto ikiwemo kama vile kuogelea, kubembea na sarakasi ambayo itafanyika kuanzia saa nne asubuhi hadi 12 jioni kwa mtonyo wa buku tatu yaani shilingi 3000.
Comments are closed.