Simba isipomuingilia Joseph Omog, itafika mbali
NI jambo zuri kwa Simba kuingia mkataba wa miaka miwili na Kocha Joseph Omog raia wa Cameroon ili aifundishe timu hiyo katika michuano mbalimbali msimu utakaonza siku zijazo. Simba imeona mbali kwani Omog anasifi ka kwa kulifahamu soka la Afrika pia Ligi ya Tanzania anaijua kwani aliifundisha Azam FC msimu wa 2013/14 bila kufungwa.
Chini ya Omog, Azam ilitwaa ubingwa wa kihistoria kwani ilikuwa mara yake ya kwanza pia haikupoteza hata mchezo mmoja, hii inatosha kuamini Simba imepata kocha bora. Tatizo linaweza kuwa lilelile la siku zote, yaani kocha kutopewa uhuru na viongozi kuingilia majukumu yake. Hakika kama kweli Simba inataka mafanikio kwa Omog, imwache hawe huru katika kazi. Kinyume na hapo Simba itabaki palepale kwani kwa kocha anayejielewa kama Omog hatokubali kuingiliwa kazi na anaweza kuiacha timu ikiwa bado inamuhitaji.


