Simulizi ya Kusisimua… MKATABA – 4
ILIPOISHIA IJUMAA
“Vipi kwani?”
“Yule matawi ya juu sana, nimeshangaa kuona mnafahamiana tena mna ukaribu.”
“Kawaida tu, yupo lakini?”
“Kwani yeye amekuelekeza lini hapa?”
“Muda kidogo, ni kama miezi minne hivi imepita.”
“Ni kweli alikuwa anaishi hapa…”
“Na sasa?”
“Amehama.”
“Amehamia wapi?”
“Soweto.”
“Dah….sijui itakuwaje sasa?” akasema kwa sauti Suma.
“Vipi ni muhimu sana kuonana naye?”
“Sana tena sana yaani.”
“Pole sana, unajua anapofanyia kazi?”
“Hapana.”
“Nitakusaidia, labda hapo unaweza kumpata.”
“Nitashukuru sana ndugu yangu.”
“Anafanya kazi Benki ya CRDB.”
“Wapi?”
“Ile iliyopo kwenye round about. Jengo la Kahawa.”
“Ahsante sana kaka, utakuwa umenisaidia sana. Ngoja nitajaribu kwenda kumwulizia pale.”
“Poa bwana.”
Suma akaondoka zake.
ENDELEA SASA…
HAKWENDA kazini. Alitaka kumpata kwanza Zakhia. Alichojua yeye ni kwamba Zakhia anafanya kazi Benki ya CRDB tu. Si zaidi ya hapo. Mawazo tele yalikuwa kichwani mwake wakati akifikiria namna ya kumpata huyo Zakhia.
Alijua wazi kwamba benki hiyo ni kubwa na kuna idara nyingi, hivyo isingekuwa rahisi kwake kufahamu moja kwa moja yupo idara gani, jambo ambalo kwa kiasi fulani lilimkatisha tamaa.
“Lakini nikiulizia watakuwa wanamjua tu…..tatizo ni kama kuna Zakhia mwingine hapo…hata akiwepo ni rahisi kumwelezea huyu ninayejua jinsi alivyo. Watakuwa wanamfahamu tu.
“Nitajua la kufanya. Mimi si mgeni hapa mjini na sidhani kama nitashindwa kujieleza kwa kiwango hicho. Nitampata tu Zakhia,” aliwaza kichwani mwake akiwa ndani ya daladala asubuhi hiyo wakati likishusha abiria katika kituo cha YMCA.
Alishukia KNCU, kisha akatembea kwa miguu taratibu jirani na Benki ya NBC, akapita katikati ya mzunguko wa mnara wa saa kisha akachepuka kidogo na kurudi kwenye Jengo la Kahawa. Alipita getini kulipokuwa na askari wawili wenye bunduki mikononi mwao.
Akaingia moja kwa moja ndani ya Benki ya CRDB. Pamoja na kwamba ilikuwa ndiyo kwanza saa 3 asubuhi, alikuta ndani ya benki hiyo kumefurika watu wengi. Wengine wakiwa wamekwenda kuhifadhi fedha huku wakiwemo waliokwenda kuchukua.
“Customer Care…” Suma alisoma maneno hayo kwenye bango dogo juu ya meza iliyokuwa na wahudumu watatu; mmoja kati yao mwanaume.
“Huyu mwanaume hawezi kunisaidia, huenda labda naye anamtaka akanikosesha bure,”akawaza Suma huku akimsogelea mhudumu mmoja wa kike, akiwa amepamba uso wake kwa tabasamu mwanana kabisa.
“Habari yako sister?” Suma akasalimia.
“Njema kabisa kaka, karibu sana.”
“Ahsante.”
“Tafadhali naomba nikusaidie.”
“Ahsante sana…samahani sana, nina shida muhimu nje ya kazi.”
“Unaweza kunieleza tafadhali.”
“Mimi naitwa Suma, ni ndugu yake na Zakhia. Najua anafanya kazi hapa, lakini sifahamu ni kitengo gani. Tafadhali dada naomba unisaidie nionane naye kama unamfahamu!”
“Zakhia?”
“Ndiyo.”
“Pole sana!”
Moyo wa Suma ukapiga kwa nguvu puuuu!
“Pole sana!” maneno hayo yakajirudia ubongoni mwake.
Alisahau kila kitu na kuanza kutafakari neno ‘pole sana’. Alishindwa kuelewa ni kwa nini alipewa pole.
Hofu ikauvaa moyo wake, picha aliyoiona mbele yake ni jeneza la Zakhia na watu wakiimwimbia huku wakimsindikiza. Uso wa dada aliyekuwa akizungumza naye ndiyo kishawishi cha fikra zote hizo. Maumivu makali yakautawala moyo wake.
“Iwe na maana yoyote ile lakini isiwe akawa amekufa…hilo tu ndiyo wasiwasi wangu na nisingependa kabisa litokee,” akawaza kichwani mwake.
Yule dada alitulia kwa muda, naye alikuwa katika kutafakari wakati akimwangalia Suma namna alivyoshangazwa na jibu lake. Alishajua alichokuwa akiwaza…
“Kwani kaka wewe unatokea wapi?”
“Nadhani hilo si la muhimu sana kwa sasa, kabla hujanieleza nini kimempata ndugu yangu.”
Kama ni kutunga uongo, Suma aliweza. Zakhia si ndugu yake bali ni mwanamke ambaye alionekana kumpenda na sasa ameamua kumfuatilia ili awe wake mke wake wa ndoa.
Akili yake haikutulia kabisa, kuna wakati alijaribu kubashiri kitu alichotaka kuelezwa na msichana aliyekuwa mbele yake. Alikuwa tayari kuambiwa chochote lakini si taarifa ya kifo.
“Tafadhali naomba uniambie, nini kimempata Zakhia?”
“Zakhia amehamishwa. Amehamia Dar es Salaam, Tawi la Vijana.”
Suma akajikuna kidevu.
Kwa hakika kidevu chake kilikuwa hakiwashi ila alilazimika kufanya hivyo. Kichwa kiliwaka moto. Ndoto zake ziliyeyuka kabisa. Alimwangalia yule dada aliyekuwa akimsikiliza kwa makini. Alitafakari jambo lingine la kumwuliza ili aweze kumsaidia.
“Dada utanisaidiaje ndugu yako?”
“Pole sana, maana ingekuwa rahisi kukupatia namba zake za simu ila sina. Wewe una simu?”
“Hapana.”
“Si unaona? Ni vigumu kukusaidia lakini kama una shida ya muhimu nakushauri nenda Dar es Salaam. Ni rahisi kufika, hilo tawi lipo eneo la Mtaa wa Lumumba, Mnazi Mmoja. Ukimwulizia pale utampata.”
“Sawa yupo idara gani?”
“Nimesikia kwamba yupo Utawala sasa hivi lakini sijui ana nafasi gani.”
“Sawa.”
Suma alitoka nje ya benki akiwa na mawazo tele. Hakutaka kwenda kazini tena. Akarudi nyumbani kwake Majengo. Haikuwa tatizo sana kutokwenda kazini siku hiyo maana alilipwa kutokana na namna anavyofanya kazi na siyo mshahara!
***
Ni siku ya nne leo anaendelea na mateso ya fikra. Suma bado hajapata uamuzi wa nini afanye. Mawazo tele yalimwandama. Hakutaka kuwaudhi wazazi wake kuhusu suala la kuoa lakini wazo lake hasa lilikuwa kuoa jini!
Potelea mbali ameamua kuoa binadamu lakini si mwingine zaidi ya Zakhia. Kitu kilichomsumbua ni eneo ambalo angeweza kumpata Zakhia.
Dar es Salaam.
Tangu kuzaliwa kwake hakuwahi kukanyaga ardhi ya Dar es Salaam, vipi angefikaje? Nani angekuwa mwenyeji wake? Nani angemkutanisha na Zakhia?
Hilo ndilo lililomtesa. Kwa lengo la kupoteza mawazo akaamua kwenda kwenye kibanda cha video kwa lengo la kupoteza mawazo na kujipa amani ya moyo wake. Naam! Sasa ameketi kwenye benchi akiangalia Sinema ya Power of Love in Hidden World (Nguvu ya Mapenzi Katika Ulimwengu Usioonekana).
Filamu hii sasa inaharibu ubongo wake. Hatua aliyopiga angalau ya kumkubali binadamu Zakhia inaanza kurudi nyuma. Hadithi ya filamu hii inamteka. Anamwona mwanaume fukara ambaye anabadilika na kuishi maisha ya furaha akimiliki fedha nyingi.
Hakupata mahali pengine popote zaidi ya msaada wa jini. Kijana huyo ambaye umri wake ulikaribia kufikia miaka 30 alionekana kung’arishwa sana na fedha za mpenzi wake jini aliyeitwa Zulfa.
Suma akatamani kuwa yeye!
“Nipo tayari kuachiwa laana, lakini mimi lazima nioe jini. Simtaki tena hata huyo Zakhia. Kazi iliyobakia sasa ni kutafuta mambo ambayo majini wanavutiwa nayo halafu nawatega. Nitampata tu!” akajisemea wakati akiendelea kuangalia sinema hiyo.
Kama ni kutekwa, Suma alikuwa ametekwa kihisia hasa. Mawazo ya Zakhia yalifia hapo. Sasa akawa na lengo moja tu; kuoa jini.
Tayari alikuwa na mbinu mpya. Kwa kuwa ndiyo aliokuwa akiwahitaji katika maisha yake, alifanya juhudi za ziada ili kugundua majini wanapenda nini. Alijihakikishia kwamba lazima angemnasa mmojawapo.
Hilo tu!
***
Suma hakuwa na muda wa kupoteza. Mkakati ulianza kutekelezwa haraka iwezekanavyo. Alikwenda kwenye duka la vipodozi na kununua perfume aina tatu kisha akaenda kwenye duka la dawa za asili na kununua marashi mengine ya aina mbalimbali na udi.
Tayari alikuwa na vifaa vya kazi. Suma alidhamiria kabisa kuwatega majini. Kwa maelezo aliyopata na jinsi alivyojifunza kupitia sinema za majini, viumbe hao walivutiwa sana na marashi ya aina mbalimbali.
Kuna nini tena?
“Tayari nina zana za kazi, wasiwasi wa nini? Watanasa tu. Suma akasema akitabasamu akiwa chumbani mwake.
Ni saa 5:45 usiku!
Saa sita kasoro!
***
Harufu kali ya udi ilizisumbua pua zake, kwa namna fulani Suma alihisi kama anapaliwa hivi. Udi nne zenye manukato tofauti zilikuwa zikifuka moshi kila upande wa chumba chake.
Muda kidogo aliona kivuli mlangoni mwake. Suma akapekecha macho ili kuangalia vizuri. Ghafla kile kivuli kilibadilika, akamuona msichana amesimama mbele yake. Kwa uzoefu wake alioupata kwa kuangalia filamu za majini, hakuchukua muda mrefu kugundua kwamba aliyekuwa amesimama mlangoni mwake alikuwa ni jini!
“Wewe ni nani na umeingiaje chumbani kwangu wakati mlango wangu niliufunga?” Suma akamwuliza msichana aliyekuwa amesimama mbele yake.
Alikuwa msichana mrembo sana, mweupe, mrefu na mwembamba kiasi lakini mwenye umbo linalofanana na tarakimu namba nane. Hakuwa na cha kumjibu zaidi ya kutembea taratibu akimfuata pale kitandani.
Kwa mara ya kwanza Suma alijishangaa kugundua kitu cha ajabu sana. Pamoja na mapenzi yake yote juu ya viumbe hao, siku hiyo Suma alimuogopa!
“Nimekuuliza wewe ni nani?”
“Mimi ni jini Suma.”
“Jini?”
“Ndiyo…tena naamini nimekuja muda mwafaka. Nina mazungumzo kidogo na wewe kama kweli unapenda majini kama ninavyokuona ukihangaika,” akasema yule msichana aliyejitambulisha kuwa ni jini akiketi kitandani.
Suma akazidi kuogopa!
ITAENDELEA JUMATANO. Kumbuka simulizi hii ni kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.
Kusoma hadithi zaidi za Joseph Shaluwa mfuatilie kwenye mitandao ya kijamii; Instagram @josephshaluwa Facebook; simulizi za joseph shaluwa