The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 12

0

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

“Anaumwa sana, madaktari wamesema hawaoni ugonjwa na hivi tunavyoongea amekata kauli, yaani wa leo wa kesho!” nilisema huku nikijisikia uchungu mkali sana ndani ya moyo wangu. Kiukweli nilikuwa nahitaji bosi huyo anionee huruma na kunisaidia.

 

SASA ENDELEA…

“Umesoma mpaka darasa la ngapi?”

 

“Form Two, nililazimika kuacha baada ya baba kuanza kuumwa na hivyo kukosa mtu wa kunilipia ada, nataka nikipata kazi nije nijisomeshe mwenyewe,” nilisema kwa adabu.

 

“Hebu chukua huu mzigo, mwaga fedha zote mezani kisha uanze kuzipanga kulinganana thamani, noti za shilingi elfu kumi zitenganishe upande wake na za elfu tano kisha utazihesabu,” alisema huku akinioneshea lile begi lililokuwa pale mezani kwake.

 

Ni begi hilo ndiyo tuliloingia nalo na wale niliokuwa nimeongozana nao wakamkabidhi, nilishtuka sana kugundua kwamba kumbe lilikuwa limejaa mabunda ya fedha.

 

Mpaka hapo sasa nilikuwa nimeshaanza kupata picha ya kinachoendelea, kwa sababu niliunganisha matukio ya milio ya risasi kusikika, wale wanaume kuja pale waliponiacha kwa kasi kubwa, kunichukua kwenye gari, kuondoka kwa kasi kama ya magari ya mashindano na mwisho kukabidhi mzigo kwa bosi.

 

Harakaharaka nilianza kufanya kazi aliyonipa yule bosi kwa sababu niliamini hiyo ndiyo inaweza kuwa tiketi ya kupata msaada kutoka kwake. Nilianza kwanza kwa kufungua fedha zote zilizokuwa kwenye mabunda, kisha nikawa natenganisha, noti za shilingi elfu kumi naziweza sehemu yake na za elfu tano mahali pale.

 

Nikiri kwamba achilia mbali kuzishika, katika maisha yangu sijawahi kuona fedha nyingi kiasi hicho. Yalikuwa ni mabunda makubwamakubwa, yakiwa yamefungwa kwa ‘rubber band’, yakiwa na mchanganyiko wa noti za aina mbili tu, za elfu tanotano na za elfu kumikumi.

 

Baada ya kumaliza kupanga, nilianza kuhesabu, nikawa nachanganyachanganya hesabu kutokana na mchecheto niliokuwa nao.

 

Ilibidi anielekeze namna ya kuhesabu, akaniambia niwe nahesabu moja moja, yaani nihesabu idadi ya noti nyekundu ni ngapi kisha nihamie zile za elfu tano. Nilihesabu mpaka zote zikaisha, yeye akawa anaandika kila kiasi ninachomwambia.

 

Kulikuwa na noti za elfu kumikumi, elfu tano na mia nne ambazo ukizipigia hesabu, ni karibu shilingi milioni hamsini na nne, na kulikuwa na noti nyingine za elfu tanotano karibu elfu tatu. Kilikuwa ni kiwango kikubwa mno cha fedha ambacho kama nilivyosema, sikuwahi kukishika katika maisha yangu.

 

Baada ya kumaliza kuhesabu, alinielekeza namna ya kuzipanga, nikawa nazifunga vizuri kwenye mabunda ya shilingi milioni kumikumi. Baada ya kumaliza, alinielekeza kukaa palepale nilipokuwa nimekaa awali kabla ya kuianza kazi hiyo.

 

“Hii kamnunulie baba yako dawa na kutimiza mahitaji mengine madogo, unatakiwa kurudi hapa kesho asubuhi na mapema, utaondoka na Bonta,” alisema huku akinipa bunda lililokuwa na karibu shilingi laki tatu.

 

Sikuyaamini macho yangu, niliinua mikono juu kamaishara ya kumshukuru Mungu, machozi ya furaha yakawa yananitoka nikiwa hata sijui nimshukuru vipi Mungu wangu. Basi Bonta, yule mwenyeji wangu aliitwa na kupewa maelekezo ambayo mimi sikuyasikia, kisha akanipa ishara kwamba nimfuate.

 

“Vipi bosi anasemaje?”

 

“Ameniambia unisindikize twende nyumbani nipeleke hizi hela za kumnunulia baba dawa kisha turudi kesho asubuhi,” nilimwambia kwa furaha.

 

“Nilikiwambia bosi wetu hana noma, cha msingi ni uaminifu tu na kubwa hutakiwi kumweleza yeyote kuhusu chochote unachokijua, kuanzia tulivyokuokoa kule mpaka ulivyokuja kuonana na bosi,” aliniambia huku tukitembea harakaharaka kutoka nje ya lile godauni kuelekea nje kabisa.

 

Nilimuahidi Bonta kwamba nitatunza siri zote na nitafanya kazi zote kwa bidii na kwa moyo wangu wote. Tulitoka mpaka kule nje kabisa ambapo Bonta alichukua pikipiki moja kubwakubwa hivi, akanipa ishara kwamba nipande, kweli nikafanya hivyo kissha tukaenda mpaka kwenye geti kubwa la kutokea ambapo alisaini kwenye daftari maalum kisha tukatoka.

 

Safari hii alikuwa akiendesha pikipiki kwa mwendo wa kawaida tu, tukaondoka nikiwa hata sijui tunaelekea wapi lakini breki ya kwanza ilikuwa ni Kipawa. Sikuwa napajua lakini mwenyewe ndiyo aliyeniambia kwamba panaitwa hivyo, siyo mbali sana na uwanja wa ndege.

 

Aliipitisha pikipiki yake kwa mafundi, akaiacha hapo kisha tukaelekea nyumbani kwake. Licha ya umri wake kuonesha kwamba anastahili kuishi na mke na watoto, Bonta alikuwa anaishi peke yake, kwenye nyumba ya vyumba vitatu iliyokuwa na kila kitu ndani kwa ndani.

 

Ilikuwa ni nyumba nzuri yenye vitu vingi vya thamani ndani, kulikuwa na televisheni kubwa ukutani, masofa ya kisasa na vitu vingine vingi lakini kasoro yake ni kwamba kulikuwa kuchafu, yaani vitu havikuwa na mpangilio.

 

“Unaweza kunisaidia kufanyafanya usafi mdogo wangu, ngoja mimi nikatafute msosi,” aliniambia na kiukweli, kutokana na mambo yote aliyonifanyia, moyo wangu ulikuwa mweupe kabisa kumsaidia chochote anachokitaka. Kwa jinsi tulivyolelewa kwenye familia yetu, nilikuwa na uwezo wa kufanya shughuli zote za nyumbani.

 

Kwa hiyo nilianza kufanya usafi mle ndani, nikafagia vyumba vyote, nikakusanya nguo zote chafu zilizokuwa zimetupwatupwa ovyo mle ndani na kuziweka kwenye kapu la nguo chafu, nikafunua mapazia yote ili hewa iingie na kuweka kila kitu sawa.

 

Baada ya hapo, nilianza kupiga deki na nilianzia kwenye chumba alichokuwa analala. Nikiwa nasogeza kitanda ili nifanye usafi mpaka chini, nilikutana na kitu ambacho sikukitegemea. Kulikuwa na bunduki iliyokatwa kitako, ikiwa imefungwa kwenye uchago wa kitanda.

 

Nilipatwa na hofu mwanzo, lakini baadaye nilipatwa na shauku ya kutaka kuitazama vizuri zaidi. Katika maisha yangu sikuwa nimewahi kuigusa bunduki hata mara moja, hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza, nikawa naichunguza vizuri huku nikitetemeka. Nikiwa naendelea kuishangaa, nilisikia mlango wa nje ukiguswa, harakaharaka nikairudisha mahali pale na kuendelea na usafi.

 

Bonta alipoingia, nilijifanya kama sijaona chochote, akawa anachekelea jinsi nilivyomsafishia nyumba yake vizuri. Aliweka chakula mezani na alikuwa pia amenunua chupa kadhaa za pombe kali, nyingine akaweka kwenye friji na akaniambia nimalizie usafi kisha ndiyo tule, yeye akawa anaendelea kunywa pombe kali.

 

Nilimalizia kufanya usafi na kumfuata, tukala pamoja chakula lakini yeye tayari alikuwa ameshaanza kulewa kwani hata mazungumzo yake yalikuwa hayaeleweki.

 

“Inabidi ukaze moyo mdogo wangu, hii kazi ngumu sana na ya hatari lakini inalipa,” aliniambia kwa sauti ya kilevi, nikamuuliza kazi gani, akacheka sana.

 

“Usiwe na haraka, kila kitu utakijua kwa undani kabisa, unachotakiwa ni kuwa na subira,” alisema, sikutaka kuhoji sana kwa sababu kama angenitazama usoni angeweza kugundua jinsi nilivyokuwa na hofu baada ya kuiona ile bunduki.

 

Kiukweli ni kwamba nilikuwa nimekosa sana amani baada ya kuiona ile bunduki, moyoni nikawa najiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.

 

Hata hivyo sikutaka sana kujali sana kuhusu kilichokuwa kinaendelea au nilichokuwa nakishuhudia, cha msingi kwangu ni kwamba nilikuwa nimefunga safari kutoka kijijini kwetu kwa ajili ua kuja kutafuta maisha na sasa kulikuwa na kila dalili kwamba nipo kwenye sehemu ambayo ndoto zangu hizo zinaweza kutimia bila wasiwasi kwa hiyo sikutaka kujishughulisha na mambo yasiyonihusu.

 

Baada ya kumaliza kufanya usafi, tulikula chakula na baada ya hapo Bonta aliniambia na mimi niende nikaoge, nikafanya hivyo na baada ya kumaliza tulipumzika kidogo mpaka majira ya kama saa mbili hivi za usiku.

 

“Tuondoke, umesema kwenu ni kijiji gani?” aliniuliza Bonta, nikamweleza kwamba kunaitwa Msanga lakini nilishangazwa na uamuzi wake wa kutaka tuondoke usiku huo. Nilipoona giza limeanda kuingia nilidhani labda ataniambia tulale mpaka kesho yake, lakini nikakumbuka kwamba bosi alikuwa amesema tunatakiwa kurejea kesho yake asubuhi.

 

“Saa hizi?”

 

“Ndiyo! Kwani hapo Msanga kuna umbali gani?” alisema huku akijiandaa ikiwa ni pamoja na kuvaa gloves maalum za kuendeshea pikipiki kwenye mikono yake. Basi sikuwa na cha kufanya zaidi ya kukubaliana naye.

 

Muda mfupi baadaye tulitoka na safari ya kuelekea Msanga ilianza kwa kutumia pikipiki yake kubwa ambayo ndiyo tuliyokuja nayo kutoka kule ofisini kwa bosi ambako mpaka wakati huo sikuwa najua kunaitwaje.

 

Wakati tunaondoka alikuwa akiendesha pikipiki kwa mwendo wa kawaida lakini kadiri tulivyokuwa tunazidi kusonga mbele ndivyo alivyokuwa akizidi kuongeza kasi, ukizingatia kwamba pikipiki hiyo ilikuwa ikipiga kelele sana, nilijikuta nikikosa amani mno ndani ya moyo wangu.

 

Pikipiki ilikuwa inakwenda kwa kasi kubwa na sikuwa na sehemu ya kushikilia zaidi ya kumshika Bonta mwilini, naye akawa anazidi kuichochea huku kwenye kona akiilaza utadhani tupo kwenye mashindano. Vile vibia nilivyokunywa viliyeyuka kutokana na hofu niliyokuwa nayo.

 

Ilifika mahali nikaona ni bora nifumbe macho nisiwe naona kilichokuwa kinaendelea kwani kiukweli mwendo aliokuwa akienda nao ulikuwa wa kutisha kwelikweli.

 

“Tunaelekea kwa wapi hapa?” aliuliza Bonta, swali lake likanifanya nifumbue macho, sikuamini kuona kwamba tayari tumeshafika Msanga. Yaani kwa mwendo tuliokuwa tukienda nao, hata kwa mtu ambaye angesafiri kwa gari asingeweza kufika kwa muda huo.

 

Nilimuelekeza na kweli muda mfupi baadaye tayari tulikuwa tukipita kwenye njia ya kuelekea nyumbani lakini safari hii tulikuwa tukienda kwenye mwendo wa taratibu kwa hiyo hata muungurumo ulikuwa wa chini. Safari iliishia nje ya nyumba yetu ambapo Bonta aliniambia kwamba natakiwa kuhakikisha ikifika saa sita, tunaianza safari ya kurejea Dar.

 

Nilimshangaa sana. Yaani tumeondoka Dar usiku, halafu tunatakiwa kusafiri tena usiku huohuo kurudi Dar, kivipi? Kila kitu kilikuwa kigeni kwangu.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube:

 

Hashpower Online. Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave A Reply