SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 20

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)
0719401968
ILIPOISHIA:
Alitufundisha kwanza kwa maneno huku akituonesha, akatufundisha namna ya kuweka risasi kwenye bunduki na kuzitoa, pia akatufundisha namna ya kuikoki, yaani kuzitoa risasi kwenye ‘magazini’ na kuziweka kwenye ‘chemba’, waliowahi kutumia bunduki watakuwa wananielewa.
Ili risasi ifyatuke, lazima kwanza uikoki bunduki na kile kitendo cha kukoki ndiyo kinachozitoa risasi kwenye ‘magazini’ na kuziweka kwenye ‘chemba’, tayari kwa kufyatua.
SASA ENDELEA…
Alitufundisha pia namna ya kutoa ‘safety lock’ na kuirudishia. Mwanzo nilikuwa najua kwamba ukipewa bunduki tu, basi wewe kazi yako ni kufyatua risasi kumbe kulikuwa na mambo mengi sana ya kitaalamu. Ndani ya muda mfupi, nilijikuta nikiwa na shauku kubwa sana ya kuishika mwenyewe kwenye mikono yangu.
Basi baada ya kufundishana kwa maneno, sasa ulifika muda wa vitendo, Mamba alituamuru kupita pale kwenye masanduku mmoja baada ya mwingine na kuchukua bunduki. Nilishangaa bunduki nyingi kiasi kile za kututosha wote, wao wanazipata wapi?
Nilichokuwa najua, ni kwamba wanaoweza kubeba bunduki, ni polisi peke yao, sasa iweje wao wawe na bunduki nyingi kiasi hicho? Wamezipata wapi? Bado kichwa changu kilikuwa na maswali mengi kuliko majibu.
Alituelekeza jinsi ya kuzibeba na akatuambia kwamba kwa sababu wengi wetu hatujui namna ya kuzitumia, tunatakiwa kuzielekezea chini ili hata mtu akifanya uzembe kwa bahati mbaya, ajipige mwenyewe miguuni. Wengi wetu tulikuwa tunatetemeka, hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kubeba bunduki.
Basi tulirudi kujipanga na safari hii, tuligeukia upande wa kule msituni ambako hakukuwa na mtu, akaanza kutuelekeza akiwa nyuma yetu, akawa anapita kwa mmojammoja na kumuelekeza namna ya kuishika na kuielekezea mbele.
Mafunzo yaliendelea kwa muda mrefu, hatimaye karibu kila mtu akawa amepata ujuzi wa namna ya kutumia bunduki. Kwa mujibu wa Mamba, hilo lilikuwa ni somo la kwanza, baada ya hapo kila mmoja alirudisha bunduki yake kwenye yale masanduku, wale wanaume wakaja na kuyabeba na kuyasogeza pembeni.
Akatuambia kwamba siku nyingine tukija, tutajifunza namna ya kulenga shabaha, nikajua basi somo limeishia hapo kumbe ndiyo kwanza limeanza. Kilichofuatia yalikuwa ni mafunzo ya ukakamavu, tulianza kwa kupiga pushapu, hapo nikajua kweli Mamba siyo mtu mzuri.
Wengi wetu hatukuwa na mazoezi ya ukakamavu kwa hiyo suala la kupiga pushapu lilikua mtihani mgumu kwelikweli. Unaweza kuchukulia rahisirahisi lakini kupiga pushapu, tena za ngumi kwa kusimamiwa siyo jambo rahisi.
Akawa akisema chini, wote tunaenda chini, akisema juu, wote tunaenda juu, tatizo likawa idadi ya pushapu tulizotakiwa kupiga. Ilifika mahali mikono yangu ikawa inatetemeka huku ikiuma mno, jasho likiwa limenitoka karibu kila sehemu.
Ugumu haukuwa kwangu pekee, nakumbuka kuna mmoja kati yetu alishindwa kabisa kuendelea, akalala chini huku akilia, Mamba akamfuata na kuanza kumpiga mateke kama mwizi huku akimtolea shombo za kutosha.
Kiukweli ilikuwa siku mbaya sana. Tulipiga pushapu zisizo na idadi mpaka ikafikia hatua kila mmoja akawa analia kimyakimya maana Mamba akikusikia unalia, ujue kazi unayo.
Lilifuata zoezi la kuruka kichurachura, nalo likawa gumu kwelikweli kwa karibu kila mtu. Tuliruka kichura mpaka ikafika mahali aliposema tusimame, ikawa hakuna anayeweza kusimama kwa kunyooka jinsi miguu inavyouma.
Bonta na wenzake walikuwa wamekaa pembeni wakiendelea kuvuta sigara na bangi kwa fujo, huku wakicheka sana jinsi Mamba alivyokuwa akituhenyesha. Tuliendelea na mazoezi mengine ya viungo na mpaka tunamaliza, kila mtu alikuwa nyang’anyang’a.
“Kesho tena tukutane hapahapa!” alisema Mamba wakati akihitimisha mafunzo, tukarudi kwenye magari huku kila mtu akiugulia kivyake, hakuna aliyekuwa na stori na mwenzake, magari yakatoka mpaka barabarani, kile kigari kidogo chenyewe kikaelekea upande tofauti na sisi, hata sijui kilielekea wapi ndani yake akiwepo Mamba na timu yake, sisi tukaanza safari ya kurudi mjini.
“Ukitaka uwe mkali, ukifika nyumbani rudia mazoezi yote mliyofundishwa, ukisema ulale, kesho utashindwa hata kuamka,” Bonta aliniambia huku akinipigapiga mgongoni, nadhani alinionea huruma kwani kila kiungo kilikuwa kikitetemeka kutokana na ‘mtiti’ tuliopewa.
Tulirudishwa mpaka kambini na mpaka tunafika, tayari giza lilishaanza kuingia, tukaenda kusaini kwenye daftari maalum kisha kila mtu akapewa shilingi elfu hamsini, tukaruhusiwa kuondoka. Bonta aliniambia hawezi kuongozana na mimi tena, natakiwa kuanza kuzoea mazingira mwenyewe.
Nilitoka nikiwa nachechemea, kilakiungo kikiuma, wenzangu nao wakawa wanaondoka kila mmoja kivyake. Nilipofika mbele kidogo, nilisimamisha bodaboda na kwenda mpaka Mombasa ambako nilipanda daladala mpaka Sinza. Mpaka naingia ndani, ilikuwa ni tayari saa nne za usiku, nikiwa nimechoka vibaya mno.
Nilichoweza kukifanya, ilikuwa ni kuoga tu, usingizi mzito ukanipitia palepale kwenye kochi nilipokaa ili kupumzika kidogo kabla ya kurudia yale mazoezi kama Bonta alivyoniambia. Nilipokuja kuzinduka, tayari kulikuwa kumeshaanza kupambazuka, nikajishangaa imekuwaje?
Nilijaribu kuinuka pale nilipokuwa nimelala lakini mwili ulikataa kabisa, viungo vyote vilikuwa vinauma mno. Ilibidi nitulie kwanza, nikashusha pumzi ndefu na kujikaza kiume, nikafanikiwa kusimama huku nikihisi kama mwili wangu unataka kupasuka kutokanana maumivu.
Ni hapo ndipo nilipoelewa ni kwa nini Bonta aliniambia kwamba nikifika natakiwa kuyarudia mazoezi yote kwanza kabla ya kulala. Kwa kuwa bado ilikuwa ni mapema sana, ilibidi nijikaze na kuanza kufanya mazoezi mepesi ili kulainisha viungo. Nilianza kwa kurukaruka taratibu, machozi yakawa yananitoka kutokanana maumivu.
Kadiri nilivyokuwa nazidi kurukaruka, maumivu yalianza kupungua na sasa viungo vikawa vinaanza kulainika, miguu ikaanza kukunjika vizuri, mikono nayo ikawa inaweza kukunjika kwa urahisi.
Nilianza kukimbiakimbia mle ndani na baada ya mwili kukaa sawa, nilirudia mazoezi yote tuliyofanya jana. Japokuwa ilikuwa bado ni asubuhi sana na kulikuw ana baridi, mwili wangu ulikuwa ukitokwa na jasho kama maji. Angalau sasa nilianza kujisikia vizuri, nikaenda bafuni kuoga kisha nikaanza kujiandaa.
Saa kumi na moja na nusu za alfajiri, tayari nilikuwa nimemaliza kujiandaa, nikatoka na kuanza kuelekea kituoni, nikapanda gari na safari ya kuelekea kambini ikaanza. Mpaka nafika, tayari ilikuwa ni saa moja kasoro za asubuhi, watu wengi tayari walikuwa wameshafika wakiendelea na kazi zao.
Kati ya wote tuliokuwa kwenye mazoezi jana, tulikuwa tumefika wanne tu, na wenzangu wote walikuwa wakichechemea kutokana na maumivu. Ile mbinu ya kufanya mazoezi asubuhi ilinisaidia sana kwa sababu angalau mimi ndiyo nilionekana kuwa ‘fiti’ japo bado mwili ulikuwa unauma kwelikweli.
Bonta aliponiona, alikuja kunisalimia huku akiwa na uso wa tabasamu, tukapeana ‘tano’ pale maana hiyo ndiyo ilikuwa salamu yetu kubwa, akaniuliza naendeleaje? Ilibidi nimsimulie kilichotokea, akacheka sana lakini akaniambia kwamba nimemfurahisha sana kwa ukakamavu niliouonesha.
Wale wengine waliendelea kufika mmojammoja na kila aliyekuwa anafika, ungeweza kudhani anaumwa kwa jinsi walivyokuwa wakiugulia maumivu. Wote tulipotimia, tulipelekwa kwenye chumba cha chini kwa chini, ambacho kilikuwa na vifaa vya kufanyia mazoezi kama ‘gym’.
Kumbe vile vyuma pale juu vilikuwa kama geresha tu, kule chini kulikuwa na sehemu kubwa ya kufanyia mazoezi ikiwa na vifaa vyote muhimu. Jamaa mmoja ambaye mara kwa mara nilikuwa namuona na Bonta, ambaye alikuwa na mwili mkubwa kwelikweli, alikuja na kuanza kutufanyisha mazoezi.
Tofauti yake ni kwamba alitufanyisha mazoezi ya kawaida tu ya kujenga mwili, na akatusisitiza kwamba tukiendelea vizuri, na sisi tutakuwa na miili iliyojengeka vizuri kimazoezi kama yeye alivyokuwa.
Niligundua pia kwamba hata mwili wa Bonta, ambao ulikuwa umejengeka vizuri sana, ilikuwa ni kwa sababu ya mazoezi maana alikuwa na kifua kipana, mikono mikubwa yenye misuli na tumbo lililotengeneza kile vijana wanachoita ‘six pack’.
Baada ya kufanya mazoezi kwa karibu saa nzima mfululizo, tulipewa muda wa kupumzika kisha tukaenda kunywa chai.
Kumbe mlemle ndani kulikuwa na kantini ambayo sikuwahi kuigundua, wahudumu wake wote walikuwa wanaume, tukapata kifungua kinywa cha nguvu kisha tukaambiwa tujiandae kwa safari ya kwenda Kazimzumbwi kumalizana na Mamba.
Watu waliposikia jina la Mamba, kila mmoja alionekana kupoteza uchangamfu usoni maana tulikuwa tunajua shughuli pevu tunayoenda kukutana nayo. Kabla hatujaondoka, kila mmoja wetu alipewa ‘ovaroli’ kama yale wanayovaa mafundi, tukavaa na kuingia ndani ya gari.
Kama ungetuona, ungeweza kudhani labda ni mafundi wa kampuni fulani wanaenda kazini lakini kumbe ilikuwa tofauti kabisa. Tulipanda kwenye magari mawili tofauti na yale tuliyotumia jana yake, na safari ya kuelekea msituni ilianza. Tulipofika, tulimkuta tayari Mamba na timu yake wameshafika, wanatusubiri, tukajipanga harakaharaka na bila kupoteza muda, kazi ikaanza.
Asubuhi hiyo tulianza kwa mazoezi ya shabaha tukiwa tumevaa maovaroli yetu, tukawekewa vitu kama sanamu za watu, zilizokuwa na michoro ya maeneo tunayotakiwa kulenga shabaha.
Alianza kwa kutufundisha kwa maelekezo kwanza huku akituonesha pia kwa vitendo, akatuelekeza sehemu za muhimu za kulenga, akatuelekeza maeneo ambayo ukimpiga mtu, unampunguza kasi ya kupambana na wewe lakini pia akatuelekeza maeneo hatari ambayo ukimpiga mtu hawezi kupona.
“Tunapoingia kazini, lazima mjue kwamba lengo letu siyo kuua watu wasio na hatia, kama tumetumwa mzigo fulani basi muhimu ni kuhakikisha mzigo unapatikana bila kusababisha vifo vya watu wasio na hatia, wananchi siyo adui zetu, adui zetu sisi ni polisi,” alisema, nikashtuka sana kusikia maneno hayo.
Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Kwa shilingi 6,000 tu unaweza kupata simulizi yote kwa mfumo wa softcopy, piga 0719401968. Pia ukitaka kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:
www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com, Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.
Usisahau kulike, share na ku-subscribe.
