The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS(USIKU WA GIZA TOTORO)-29

0

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

Baada ya hapo, alituamrisha wote kuingia kwenye jengo kubwa kama bwalo hivi, mle ndani mlikuwa kama ‘gym’, kulikuwa na vyuma vingi vya kufanyia mazoezi na vifaa vingine vingi, tukanyanyua sana vyuma zamuzamu huku akipita kukagua kwa karibu kuona kama kila mtu anafanya kile alichoambiwa.

SASA ENDELEA…

Zoezi la mwisho, lilikuwa ni la ‘ku-craw’, haya mazoezi huwa wanayafanya sana wanajeshi, mnalala chini na kuanza kujivuta kwa kutumia tumbo huku ukitumia viwiko vya mikono.

 

Alitupeleka kutambaa umbali mrefu sana, wakati mwingine tukipita kwenye mifereji, kwenye miba, kwenye kokoto mpaka mimi ikafika mahali nikawa nahisi tumbo na viwiko vya mikono vinavuja damu.

 

Mpaka tunamaliza, ilikuwa tayari ni alfajiri, kengele ikagongwa tena mara moja kama mwanzo, tukarudi na kwenda kujipanga palepale tulipoanzia, Gamutu akawa anatoa maelekezo.

 

“Usiku wa leo kuna kazi! Mtakaochaguliwa mtajulishwa mapema, ambao hamtachaguliwa kutakuwa na mazoezi ya kulenga shabaha, atakayeleta masihara tutamuweka yeye kama sehemu yakujifunzia shabaha, wale wenye mikono yote ya kushoto muanze mazoezi mapema,” alisema kibabe kisha akatoa ishara ya wote kutawanyika.

 

“Vipi mshkaji wangu, uko vizuri kinoma. Nilikuwa nakufuatilia,” Kezia aliniambia wakati nikitembea kichovu kurudi chumbani kwangu, tukacheka kichovu maana wote tulikuwa tumechafuka na kuchoka vibaya.

 

Hatukuwa na stori nyingi, tukaagana na kilammoja akaenda kwenye chumba chake. Nilielewa kwa nini Kezia muda niliofika aliniambia kwamba amechoshwa na maisha ya pale gerezani. Ilikuwa ni zaidi ya kambi ya jeshi, zaidi ya gereza.

 

Kwa mazoezi yale, nilielewa ni ugumu gani polisi wanakabiliana nao kwa sababu kwa mazoezi yale, mkienda kufanya tukio halafu mkakutana na polisi wachovu, mnaweza kuwafanyia kitu kibaya sana.

 

Yalikuwa ni mazoezi magumu na ya kuchosha sana ambayo hata kama ulikuwa na moyo mzuri kiasi gani, yanakubadilisha na kukufanya uwe na roho ya kikatili. Nilipoingia ndani kwangu, nilifikia bafuni, nguo zilikuwa hazitamaniki, ikabidi nianze kwanza kuzifua, kisha na mimi nikaoga na kujisafisha vizuri.

 

Mpaka narudi kitandani kupumzika, ilikuwa ni tayari saa kumi na moja alfajiri. Nilipojilaza tu, nilipitiwa na usingizi mzito, nilikuja kuzinduliwa na mtu aliyekuwa akigonga mlango.

 

Niliamka kichovu nakutoka, alikuwa ni yule mzee wa chakula, alikuwa ameleta kifungua kinywa. Kilikuwa ni kifungua kinywa cha nguvu, supu, chapati nne na vikorombwezo vingine kibao.

 

“Wewe ni mgeni? Sura yako ni ngeni kwangu,” aliniambia yule mzee, nikamjibu kwamba ni kweli mimi ni mgeni na ndiyo kwanza nilikuwa nimefika jana yake tu.

 

“Utapaweza kweli hapa? Maana shughuli ya hapa si ya kitoto,” aliniambia huku akitabasamu, sikumjibu zaidi ya kutabasamu kichovu maana alichokuwa anakisema tayari nilishaanza kukiona. Basi akaniachia kifungua kinywa na kuondoka zake.

 

Alipoondoka tu, Gamutu alikuja na kunigongea, nikapata bahati ya kumtazama vizuri. Hata sijui nimuelezee vipi, lakini kwa kifupi aliniambia kwamba na mimi nimepangwa kwenye kazi ya usiku kwa hiyo nijiandae.

 

Mapigo ya moyo yalinifyatuka paaah! Moyo ukaanza kunidunda, nikajua mwisho wangu umewadia.

 

Kumbukumbu za tukio la kwanza tulilolifanya kule Tandika, zilikuwa zikipita kwa kasi ndani ya kichwa changu, nikawa nasikia milio ya risasi, nikawa nawaona wale wenzangu wawili jinsi walivyochakazwa na risasi na kupoteza maisha, mmoja palepale eneo la tukio na mwingine ndani ya gari!

 

Japokuwa kulikuwa ni baridi, nilijihisi kijasho chembamba kikinitoka. Gamutu aliondoka na kuniacha nimesimama palepale mlangoni, mawazo mengi yakiendelea kupita ndani ya kichwa changu.

 

“Oya vipi mwanangu, mbona unambwelambwela hapo?” sauti ya Kezia ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye lindi la mawazo, nikalilazimisha tabasamu kwenye uso wangu.

 

“Daah! Mwanangu jana bado kidogo nibambwe, lile dubwasha sijui lingenifanya nini maana huwa linanitongoza kila siku nalikimbia,” alisema Kezia kwa mbwembwe na kunifanya nishangae. Stori zake kidogo zilinisahaulisha jambo zito lililokuwa mbele yangu.

 

Tuliingia ndani, Kezia akaendelea kunipa michapo kuhusu yeye na Gamutu na jinsi anavyomfanyia visa baada ya kukataa kuwa naye kimapenzi.

 

“Ujue mimi hapa napata sana shida sema kwa sababu nimeshakuwa na roho ya korosho, najua namna ya kushughulika na mijitu kama gamutu,” alisema Kezia huku akicheka na kujitupa kitandani kwangu.

 

Nilishangaa sana kusikia Gamutu pamoja na ubabe wake wote, kumbe na yeye alikuwa akimtaka Kezia kimapenzi. Kama nilivyoeleza, Gamutu alikuwa na mwonekano wa kutisha kwelikweli, yaani ile taswira halisi ya jambazi ulikuwa unaweza kuipata kwa kumtazama.

 

Alikuwa mrefu, mwenye mwili mkubwa halafu usoni ana makovu makubwamakubwa, midomo yake imebadilika rangi na kuwa myeusi, nadhani ni kwa sababu ya kunywa pombe kali na kuvuta sana sigara na macho yake yalikuwa mekundu sana nadhani ni kwa sababu ya kuvuta ‘mibange’.

 

“Lakini nampendea kwenye kazi, akiwaongoza kwenye ‘misheni’, anasimama mwenyewe mstari wa mbele na akishika chuma huwa hana masihara hata kidogo,” alisema Kezia na kunielezea jinsi ilivyokuwa kwenye matukio kadhaa aliyowaongoza.

 

“Nimeambiwa na mimi leo nitakuwa miongoni mwa watakaotoka usiku, yaani hapa nimechanganyikiwa kwelikweli,” nilimwambia Kezia, akacheka sana na kuniambia kwamba mwanzo mgumu, baadaye nitazoea na nitakuwa siogopi tena.

 

Maneno yake kidogo yalinifariji, tukaendelea kupiga stori za hapa na pale, tukikumbushiana tuliyoyafanya jana. Stori ziliendelea mpaka muda wa chakula cha mchana ambapo yule mzee aliponiletea cha kwangu, Kezia alimwambia na cha kwake pia amletee palepale kwangu, jambo ambalo alilikubali.

 

Tulikula chakula na Kezia, tukipiga stori nyingi na kucheka sana, tulipomaliza, Kezia alianza uchokozi wake tena, mwisho tukajikuta tukiwa kitandani. Alikuwa mwalimu mzuri sana kwangu na kadiri tulivyokuwa tukiendelea, ndivyo nilivyokuwa nikizidi kujifunza mambo mengi ambayo awali sikuwa nayajua.

 

Ukichanganya shibe na uchovu, tulijikuta tukipitiwa na usingizi palepale tukiwa tumelala kihasarahasara. Kilichokuja kunizindua, ni baada ya kusikia mlango ukigongwa kwa nguvu, nikakurupuka na kuanza kutafuta nguo zangu, Kezia akiwa bado ameuchapa usingizi.

 

Kibaya ni kwamba kumbe yule mzee alipoleta chakula, hatukukumbuka kufunga mlango, kwa hiyo aliyekuwa anagonga, alipoona kimya alijaribu kunyonga kitasa, kweli mlango ukafunguka.

 

Nilishtuka mno kugundua kwamba kumbe aliyekuwa akigonga alikuwa ni Gamutu, macho yangu na yake yakagongana, nikamuona akihamishia macho yake haraka kwa Kezia ambaye bado alikuwa amelala.

 

“Ahaaa! Kumbe ndiyo mchezo mnaoufanya huu,” alisema Gamutu huku akianza kuchomoa mkanda wa kijeshi kwenye suruali yake. Sauti yake ilimzindua Kezia kutoka usingizini, naye akakurupuka na kuanza kutafuta nguo zake.

 

“Tulia hivyohivyo,” alisema Gamutu huku akifunga mlango kwa ndani na kutusogelea. Kezia alikuwa ameshavaa skin tight yake, akakurupuka huku akiwa amejifunika shuka na kusimama mbele yangu huku akihema kwa nguvu.

 

“Gamutu please, naomba usifanye jambo lolote, mimi na wewe tutazungumza baadaye,” alisema Kezia kwa sauti ya kubembeleza, Gamutu akamtazama kwa sekunde kadhaa kwa macho ya ukali, nikamuona akifumba macho yake kidogo na kuyahamishia kwangu, akanitazama huku akihema kisha akashusha pumzi ndefu, Kezia akawa anaendelea kumsihi atulie watayazungumza.

 

Katika hali ambayo sikuitegemea, nilishangaa kumuona Gamutu akiurudishia mkanda wake kiunoni, kisha akageuka na kutaka kutoka nje, alipoufikia mlango akawa ni kama amekumbuka kitu.

 

“Jiandae tunaenda kwenye maandalizi ya mwisho sasa hivi, nakupa dakika mbili,” alisema kisha akafungua mlango na kutoka, akaubamiza kwa nguvu, mimi na Kezia tukawa tunatazamana.

 

“Nisamehe, mimi ndiyo mwenye makosa,” alisema Kezia na kwenda kufunga mlango kwa ndani, akaja na kunikumbatia kwa nguvu huku akinibusu sehemu mbalimbali za mwili wangu.

 

“Mkienda naye kwenye kazi kuwa makini, anaweza kukufanyia makusudi kulipa kisasi, nitajaribu kuzungumza naye kabla hamjaondoka, najua namna ya kumtuliza,” alisema, akaniachia na kuanza kuvaa nguo zake, na mimi nikavaa za kwangu na kuanza kujiandaa kama alivyoniambia.

 

Harakaharaka Kezia alinibusu tena na kwenda kufungua mlango, akatoka na kuniambia anataka kabla hatujaondoka tuonane, nikatingisha kichwa kumkubalia, moyoni nikaanza kuwa na hofu kwa sababu kweli Gamutu angeweza kunifanyizia.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia: www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online. Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

 

 

Leave A Reply