The House of Favourite Newspapers
gunners X

Trump Ajiondoa Marekani Kwenye Mashirika 66 ya Kimataifa

0
Rais wa Marekani, Donald Trump

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameagiza nchi yake kujitoa katika mashirika 66 ya kimataifa, akieleza kuwa taasisi hizo hazihudumii tena maslahi ya taifa la Marekani. Uamuzi huo umeainishwa katika hati ya maelekezo aliyosaini jana Jumatano, Ikulu ya White House ikisema hatua hiyo inaendana na sera ya “America First” inayolenga kuweka mbele maslahi ya ndani ya nchi.

Kwa mujibu wa Ikulu, mashirika 31 kati ya hayo ni ya Umoja wa Mataifa (UN), huku mengine 35 yakiwa ni taasisi zisizo za UN. Mashirika mengi yaliyoathiriwa yanajihusisha na masuala ya mabadiliko ya tabianchi, utawala wa kimataifa, ajira na maendeleo.

Utawala wa Trump umeeleza kuwa maeneo hayo yanachochea ajenda wanayoitaja kama “woke”, ambayo, kwa mtazamo wao, haipatani na vipaumbele vya Marekani. Miongoni mwa taasisi za UN zilizoathiriwa ni tume za kiuchumi na kijamii za Afrika, Asia-Pasifiki, Amerika ya Kusini na Karibiani, pamoja na UN Trade and Development (UNCTAD), International Trade Center (ITC) na International Law Commission (ILC).

Hatua hiyo pia inahusisha mashirika makubwa yasiyo ya UN, yakiwemo Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), Shirika la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA), pamoja na majukwaa mbalimbali ya kimataifa yanayoshughulikia uhamiaji, mapambano dhidi ya ugaidi na nishati safi.

Uamuzi huu unakuja wakati Rais Trump akikaribia kutimiza mwaka mmoja tangu kuanza kwa muhula wake wa pili madarakani. Tangu arejee Ikulu, tayari amechukua hatua za kujitoa katika Shirika la Afya Duniani (WHO), Mkataba wa Tabianchi wa Paris na UNESCO, maamuzi ambayo yameongeza mvutano kati ya Marekani na washirika wake wa kimataifa, hususan ndani ya muungano wa NATO.

Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema hatua hiyo inaweza kuwa na athari kwa ushirikiano wa kimataifa, hasa katika masuala ya tabianchi, biashara na usalama wa dunia, huku White House ikisisitiza kuwa maslahi ya Marekani ndiyo kipaumbele kikuu cha utawala wa sasa.

”NAKUPA SIKU 7 NENDA KABOMOE – MKABIDHI MAMA ENEO LAKE” – WAZIRI MKUU AINGILIA KATI MGOGORO ARDHI

Leave A Reply