The House of Favourite Newspapers
gunners X

Tundu Lissu Atengua Uteuzi wa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema Catherine Ruge

Catherine Ruge

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Tundu Lissu, leo Jumamosi Aprili 05, 2025 ametangaza kutengua uteuzi wa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema na Mtaalamu wa dawati la Jinsia wa Chama hicho makao makuu, Bi. Catherine Ruge kuanzia leo Aprili 05, 2025.

Taarifa hiyo imechapishwa kwenye mitandao ya Kijamii na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa mawasiliano wa Chadema Bi. Brenda Rupia, siku moja mara baada ya kuchapishwa kwa waraka wa kundi linaloitwa G55 ambalo Catherine Ruge ameonekana kuwa mwanachama wake, likijumuisha pia waliokuwa watia nia ya ubunge mwaka 2020 na 2025.

Wanachama hao walitangaza hadharani kupingana na maamuzi ya Chadema Taifa ya kutoshiriki katika uchaguzi Mkuu ujao na hivyo kwenda kinyume na azimio la Chama la “No Reforms, No election” lenye kutoa msimamo wa kutofanyika kwa uchaguzi ikiwa hakuna Mabadiliko ya kisheria na kimfumo katika usimamizi na uendeshaji wa uchaguzi mkuu.

Catherine Ruge ambaye alikuwa Katibu wa Baraza la wanawake Chadema kwenye uongozi uliopita, anaungana na Ndugu Julius Mwita aliyeondolewa kwenye nafasi yake ya Katibu wa Sekretarieti ya Chadema mwanzoni mwa Juma hili, kutokana na misimamo yake kwenda kinyume na maazimio ya Chadema ikiwa ni pamoja na kupingana na maazimio ya Chama chake.

Katika Waraka wao wa pamoja kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika Ruge na wenzake wanaamini kuwa haitowezekana kuzuia uchaguzi Mkuu ujao kwa Chadema kuwa nje ya uchaguzi huo, wakisema matokeo yake yatakuwa ni kufunguliwa mashtaka ya jinai na kujipata kwenye misukosuko ya mamlaka zinazohusika na uchaguzi.

“Kujaribu kuuzuia uchaguzi tukiwa nje ya uchaguzi itakuwa ni sawa na kufanya jinai. Uwezekano pekee wa kuzuia uchaguzi ni kushiriki uchaguzi kwa kuhakikisha tunaingiza wagombea katika uchaguzi na ni rahisi wagombea kuhamasisha na kuongoza wananchi kuzuia uchaguzi kwenye vituo hasa katika majimbo na kata zenye kuelekea kufanyiwa hujuma kuliko kujaribu kuzuia uchaguzi wote tukiwa nje.” Imesomeka sehemu ya waraka huo.

Comments are closed.