Ukiona huna nafasi Yanga SC, ruksa kuondoka
Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam
YANGA jeuri sana eti imesema kama kuna mchezaji anaona hana nafasi katika kikosi cha kwanza na anahisi uwezo wa kuingia ‘first eleven’ ni mdogo huku akiwa hana raha klabuni, kiroho safi anaweza kuondoka.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tu baada ya baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wasio na nafasi katika kikosi cha kwanza kudai hawana amani klabuni hapo. Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro ameliambia Championi Jumamosi kuwa, mchezaji yeyote anayeona ameshindwa kupambana kikosini ni ruhusa anaweza kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine ambako anaweza kucheza.
Alisema anachotakiwa kufanya mchezaji wa aina hiyo ni kuwasiliana na uongozi wa Yanga ili uweze kumpatia ruhusa na siyo kuanza kulalamika pembeni. “Yanga ni kama bahari, anayeweza kupiga mbizi ndiye anayeweza kuvuka atakayeshindwa anaweza
kuomba boya au akaogelee katika bwawa la kuogelea.
“Kama kuna mchezaji kaona hawezi kwenda na kasi ya Yanga ni bora akaomba aruhusiwe kuondoka akatafute timu ambayo anaona kuwa anaweza kuendana na kasi yake kuliko kukaa na kuanza kutoa lawama zisizokuwa na faida,” alisema Muro. Tayari Yanga imeshamruhusu Paul Nonga kujiunga na timu nyingine baada ya straika huyo kuomba kuondoka kutokana na kushindwa kupata nafasi mbele ya Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Malimi Busungu.


