UVCCM Kibiti Yampaisha Rais Samia Huku Mwenyekiti Wake Akijivunia Mafanikio

PWANI, Kibiti Jumatatu 14 Marchi 2022 Umoja wa vijana CCM (UVCCM) Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani leo wametoa pongezi za dhati kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Taifa kwa jinsi anavyoendelea kuchapa kazi huku umoja huo ukihaidi kuendelea kufanya kazi naye bega kwa bega ili kuhakikisha maendeleo ya nchi yanasonga mbele pamoja na kuendelea kufanya kazi kwa nguvu zote na kuendelea kuimarisha Cha Cha Mapinduzi (CCM).
Hayo yamesemwa leo wilayani Kibiti na Mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya hiyo Juma Kassim Ndaruke wakati wa kikao cha Baraza Kuu UVCCM kilichokuwa na agenda ya kujadili taarifa ya mwaka 2021 kuanzia Januari mpaka Disemba pamoja na mafanikio ya umoja huo kwa miaka mitano iliyopita.

‘Kwa niaba ya UVCCM Wilaya ya Kibiti, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio yake ya mwaka mmoja madarakani pamoja na kazi kubwa alioifanya kwa wilaya yetu kwani kwa mwaka huo mmoja, aliweza kuleta fedha za maendeleo kwa wilaya ya Kibiti jumla ya Tzs 2.3bn ambazo kwa kiasi kikubwa zimeweza kujenge madarasa na kufanya watoto kusomea kwenye mazingira rafiki,’ Alisema Ndaruke.
Ndaruke aliongeza, ‘Sisi kama vijana ambao tunapenda maendeleo tulihakikisha ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia, tulishiriki kwa nguvu zote kuhakikisha zinatumika ipasavyo na pia tulikuwa tunajitolea kwenye ujenzi wa madarasa ya watoto wetu kwa kushiriki kwenye ujenzi kama vile kuchimba msingi wa kujenga madarasa’.
Kuhusu mafanikio ya UVCCM wilaya ya Kibiti kwa kipindi cha miaka mitano, Mwenyekiti huyo ambaye anamaliza muda wake alisema kuwa uongozi uliopo ulichanguliwa mwaka 2017, na kwa wakati huo jumuiya ilikuwa ni dhaifu sana kiuchumi kuanzia ngazi ya mashina mpaka wilayani hali iliyopelekea kukwama kwa utekelezaji wa mipango mingi ambayo ingekuwa na manufaa kwa chama na wananchi wa wilaya ya Kibiti.
Ndaruke alisema, ‘Kwa pamoja tuliamua kuweka mpango mkakati wa kuimarisha jumuiya ya vijana kwa wilaya kwa kuweka malengo ya kuamsha hali ya vijana kushiriki shughuli za kisiasa, kuamsha hali ya vijana kushiriki na kujitolea katika shughuli za maendeleo, kuinua hali ya uchumi kwa vijana pamoja na jumuiya na kukisaidia chama kuendelea kuhudumia wananchi na hatimae kushinda changuzi zote’.
‘Ninayo furaha kwa siku ya leo kusema kuwa kwa mipango yetu hiyo tulianza kupata matokea chanya kwani ili kuwapa vijana hamasa tulianzisha programu ya kambi ya vijana ambapo vijana Zaidi ya 500 walishiriki na kunufaika na mafunzo pamoja na kutengeneza kikundi cha hamasa kwa vijana na kupata mafanikio ya kushika nafasi ya pili kimkoa kwenye mbio za mwenge za mwaka 2021 kutokana na ushirika wake yakinifu’.
Ndaruke aliongeza, ‘Kwenye kuendelea kuimarisha chama, tuliweza kuzindua mashina mapya Zaidi ya 30 katika kata mbali mbali ndani ya wilaya na kusaidia kuongeza idadi ya wanachama na kuhimarisha uhai wa chama kwa kiasi kikubwa’.
Na ili kuendelea kuunga mkono serikali yetu iliyopo madarakani, tuliweza kuweka mkakati wa kutengeneza vikundi vya vijana kupitia mashina yao ambapo jumla ya vikundi 85 tulitengeza na kunufaika na Tzs 250,630,028 ambazo zilitolewa kwao kama mkopo na halmashauri, alisema Ndaruke huku akisema kuwa uongozi wake unajivunia kwa matokeo hayo kwani kwa sasa vijana wengi ndani ya wilaya ya Kibiti wana ari ya kushiriki katika siasa huku jumuiya hiyo ikiwa na uwezo wa kujiendesha yenyewe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti ambaye alikuwa mgeni rasmi Kanali Ahmed Abbas alimpongeza Mwenyekiti wa UVCCM Kibiti Ndukule kwa juhudi kubwa ya kuwaleta vijana pamoja na kushiriki kwenye kazi za maendeleo na hivyo kufanya kazi ya serikali kuwa rahisi.
Napenda kutoa shukrani za dhati kwa Mwenyekiti wa UVCCM na ambaye anamaliza muda wake kwa kujitoa kwake na kuweza kuwaleta vijana pamoja lakini Zaidi kwa kufanya vijana kuwa kiungo muhimu kwenye kufanikisha shughuli za serikali. Mimi kama kiongozi wa serikali wa wilaya hii nimefanya kazi pamoja naye kwa mafanikio makubwa, ni kijana mwenye ari ya kufanya kazi na kila mtu na pia kwa tabia yake ya kushirikiana na viongozi wote wa wilaya. Nachukua nafasi hii kumtakia kila la kheri na aweze kupata nafasi ya juu kuliko hii alioiacha.
Kanali Abbas alichukua fursa kuwaomba wananchama wote wa CCM kujiweka tayari kwa ajili ya uchanguzi wa jumuiya zake ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu.
Wilaya ya Kibiti kwa sasa ina umri wa miaka 6 baada ya kurasimishwa rasmi mwaka 2016 ambapo ilizaliwa kutokea kwenye wilaya ya Rufiji. Mwaka 2017 uchanguzi wa chama ulifanyika na ndipo uongozi uliopo ulichanguliwa na kufanya kuwa uongozi wa kwanza kwa jumuiya ya UVCCM.

