Wanaharakati Walia Mbunge Kutolewa Nje Kisa Nguo
Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini yamekosoa hatua ya Spika wa Bunge Job Ndugai kumtoa nje Mbunge wa Momba, Condester Sichalwe kutokana na kuvaa suruali iliyombana.
Mashirika hayo yamesema maamuzi ya kumwamuru mbunge huyo kuondoka ndani ya ukumbi wa Bunge yanaonekana kuwa na walakini mkubwa maana mavazi yake hayakuwa na kasoro yoyote.
Akizungumza na GLOBAL, Mkurugenzi wa Kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC), Anna Henga alisisitiza kuwa nguo aliyokuwa amevaa mbunge huyo haikuwa na tatizo lolote kwa sababu ilimsitiri vema na ilikuwa nguo ya heshima.
“Na nguo kama hizo zimekwishawahi kuvaliwa na naibu spika, zimeshawahi kuvaliwa na wabunge wengine, na hata yeye amekwishawahi kuvaa nguo kama hiyo… kwa hiyo sisi tunaona kwamba kanuni hizi ama zina changamoto ya tafsiri au mtu yoyote anaweza kutafsiri vazi la heshima maana yake ni nini au pia wanawake wanaonekana kama ni kitu ambacho kinaweza kudhalilishwa kwa namna yoyote ile” alisema Henga.
Henga alisema hatua kama hiyo ikiendelea itawaondolea ujasiri wanawake bungeni.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mratibu wa Mtandao wa wanawake watetezi wa haki za binadamu Tanzania, Hilda Stuart ambaye alisema mtandao huo umepitia kanuni za Bunge sehemu ya 170 inayoelekeza mavazi wanayopaswa kuvaa wanawake wabunge au wanawake wanaoingia bungeni na kuona kuwa mavazi aliyovaa Condester hayakuwa na kasoro yoyote kama ilivyodaiwa na mtoa taarifa kwa Spika wa Bunge.
Alitoa wito kwa Bunge kuchukua tahadhari zote za kuzuia vitendo vya udhalilishaji wa wanawake kwa lengo la kuwakandamiza ili kuwaondolea ujasiri wawapo bungeni.
“Udhalilisha wa wanawake una madhara makubwa katika jamii na unadhoofisha ukuaji wa maendeleo hususani kufikia maendeleo endelevu . Suala la udhalilishaji wa wanawake pia linarudisha nyuma lengo la kufikia usawa wa kijinsia, ambao unatakiwa kupewa kipaumbele ili kufanikisha lengo la maendeleo endelevu ya 2030,” alisema.
Juni Mosi mwaka huu, Mbunge wa Nyang’wale (CCM), Hussein Amar aliomba mwongozo wa Spika kwamba mbunge Condester alikuwa amevaa mavazi yasiyo na staha bungeni.
@gabriel mushi