Wanaoiua Singeli Ndiyo wa Kuiokoa
ZAIDI ya miaka miwili iliyopita, hali ya muziki wa Singeli ilikuwa njema sana kuliko ilivyo leo hapa nchini.
Ni katika kipindi hicho baadhi ya wadau walidhani muziki huo ulikuwa tishio kwa ufalme wa Bongo Fleva.
Dhana zao zilitokana na namna watu walivyoupokea muziki huo.
Kishindo chake kilikuwa kikubwa hadi kuwafanya baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva kuanza kujiandaa kisaikolojia kwa wao kuweka vionjo vya Singeli kwenye ‘biti’ na tungo zao.
Vyombo vya habari navyo havikubaki nyuma, vilianza kuzipiga nyimbo za Singeli kwa sifa huku baadhi vikijinasibu kuwa ni vyombo vya habari vya kisingelisingeli.
Ila mimi niwe wazi sikutikiswa hata kidogo na kishindo cha Singeli kwa sababu naifahamu vyema historia ya muziki wa Bongo na hasa huu wa kizazi kipya.
Muziki wa Bongo Fleva una historia yake na ina msisimko wa kipekee. Siyo muziki uliokuwa kwa kasi ya uyoga na kujikuta ukikubalika.
Wakati Bongo Fleva inaaza watu waliohusika na muziki huu walikosa thamani mbele ya jamii, walishindwa kuheshimika wala kupata faida ambayo walidhani wangeipata kwa wao kuwa wasanii.
Vizazi tofautitofauti vya wanamuziki wa Bongo Fleva vilipita na jasho lao la kutafuta soko liliwakaukia wasanii wenyewe bila kuleta faida kwao.
Baadaye kizazi cha akina Sugu, Juma Nature na Profesa Jay viliibuka; vikatengeneza njia ya muziki huo kukubalika kutokana na aina yao ya uimbaji na kughani mashairi.
Juhudi zao hatimaye zilileta mafanikio hadi leo siyo tu muziki huo unakubalika sana ila umekuwa chanzo kikubwa cha utajiri kwa baadhi ya wadau na wanamuziki wenyewe.
Singeli hawana historia hii. Singeli bado wako katika hatua ya mwanzo kabisa ambayo wana Bongo Fleva walianza nayo.
Iangalie Singeli ya leo; bado wanamuziki wake wanasifia uhuni na fujo.
Bado muziki wao unaonekana ni wa tabaka fulani la uswahiliniswahilini; ni njia ileile ambayo Muziki wa Bongo Fleva ulipita zamani.
Leo siyo ajabu wala haishangazi kumuona mtu akisikiliza muziki wa Bongo Fleva barabarani lakini vipi ukikutana na msichana mrembo halafu anasikiliza au kuimba Singeli utamwelewaje?
Wanamuziki wa Singeli inabidi wabadilike na kujua mwanzo ilikuwa vema kutumia mtindo wa kihunihuni ili kupata mashabiki; ila baada ya kuwapata ilitakiwa wabadili gia angani na kufuata mahitaji ya watu na ustaarabu wao kama wenzao wa Bongo Fleva walivyofanya wakati ule ‘wanahaso’ kupata heshima ya muziki wao.
Kuendelea kushabikia uhuni, ngono na mambo yasiyofaa katika muziki wao, siyo tu unasababisha muziki huo uchelewe kwenda mbele ila pia unafanya muziki huo kushindwa kupata mashabiki wapya na hivyo kuusogeza kwenye kifo.
Wapo wanamuziki wachache wa Singeli wanaojitahidi kubadilika na kutaka kuonesha thamani na hali ya muziki huo, ila wengi wao bado wanaamini Singeli ni muziki wa kihuni.
Nilifurahi kuona mapema tu wakina Msaga Sumu na wenzao wakianza kumiliki magari na kuishi kutokana na muziki wao. Wenzao wa Bongo Fleva haikuwa rahisi hivyo.
Wao walipigika, waliteseka kwa miaka mingi na bado hawakuambulia chochote.
Wachache walioonekana kumiliki magari basi yalitokana na kazi zao nyingine ama fadhila za familia zao, hasa kwa wale waliotoka katika familia za kipato cha juu.
Kuna dalili ya muziki wa Singeli kukubalika baadaye; ila siyo kazi rahisi.
Inabidi wanamuziki wake wajipange na kubadilisha mtazamo hasi uliojengeka vichwani mwa watu kuhusu muziki huo.
Wawe wabunifu na wajue ubora wa muziki wao ndiyo thamani ambayo wamekuwa wakiitamani miaka yote.
Wajue ipo tofauti kati ya wao kujulikana na kazi zao kukubalika kwenye jamii. Mtu yeyote anaweza kujulikana ila akawa hakubaliki.
Niwashauri wasanii wa Singeli wasiridhike na mafanikio madogo waliyopata wakajiona wamemaliza kazi, bado wanayo kazi ya kuufanya muziki wao uweze kusikilizwa na wengi bila ubaguzi.
Inabidi waumizwe na hali ya muziki wao kuonekana ni wa kihuni na uliokosa maadili na kwamba wanaoushabikia ni watu wahuni.
Iko hivi; wanaoiua Singeli ndiyo haohao wanaoweza kuinusuru isife.
Kazi ya kufanya muziki wa Singeli ukubalike iko kwa wanamuziki wenyewe. Iko kuanzia katika midundo mpaka mashairi.
Iko kuanzia staili ya kucheza mpaka mavazi. Huko ndiko panapotakiwa kuangaliwa vizuri na kurekebishwa.
Muziki wa Singeli una nafasi kubwa mno ya kukubalika ikiwa wanamuziki wake wakiamka na kujua wapi wanakosea na hivyo kuparekebisha mapema.
Hizi ni salamu zangu kwa wasanii wote wa Singeli, Sholo Mwamba, Dula Makabila, Mzee wa Bwax, Man Fongo, Skide Masai wa Kigoma na Msaga Sumu, wakiona zinafaa wazipokee kama hazifai wazipotezee!