Wanawake 46 Wauawa Kwenye Gereza la Wanawake Nchini Honduras

Takribani Wanawake 46 wameuawa katika ghasia iliyozuka kwenye Gereza la Wanawake nchini Honduras.
Walionusurika katika tukio hilo wameeleza kuwa mapigano hayo yalianza kutokana na mashindano kati ya magenge pinzani kutoka kwenye mashirika mawili yenye uhalifu mbaya kuliko yote Amerika ya kati.
Ndipo genge mojawapo lilipowasha moto kwenye sehemu ya Gereza hilo wanapoishi wapinzani wao.
Maafisa wanasema wanawake wengi wamepoteza maisha kutokana na kuungua moto huku wengine wakipigwa risasi, kuchomwa na vitu vyenye ncha kali au kupigwa mpaka kufa.
Uchunguzi juu ya tukio hilo bado unaendelea ili kubaini wafungwa hao waliwezaje kupata silaha za moto na mapanga ndani ya gereza.
Kupitia mitandao ya kijamii Rais Xiomara Castro ambaye mwaka jana alianzisha kampeni ya kukamata magenge ya kihalifu amesema ameshtushwa na mauaji ya kinyama ya wanawake hao na ameahidi kuwa hatua kali zitachukuliwa.
Kwa kuanzia , Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Ramon Sabillon amefukuzwa kazi na nafasi yake amepewa Mkuu wa Jeshi la polisi, Gustavo Sanchez.

