Waziri Mkuu wa Ufaransa, Sebastien Lecornu, Ajiuzulu Wiki Chache Baada ya Kuteuliwa

Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa, Sebastien Lecornu, amejiondoa madarakani leo, Oktoba 6, 2025, ikiwa ni wiki chache tu baada ya kuteuliwa kwake, na kuingiza nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa mpya.
Taarifa ya kujiuzulu kwake imebainisha kuwa Lecornu anakuwa Waziri Mkuu wa tano wa Ufaransa kuchukua uamuzi huo ndani ya kipindi cha chini ya miaka miwili.
Ripoti zinaonyesha kuwa Lecornu alikabiliwa na changamoto kubwa ya kuishawishi bunge lililogawanyika ili kupitisha bajeti ya mwaka 2026, jambo ambalo lilionekana kuwa gumu kutokana na migawanyiko ya kisiasa na tofauti za sera.
Waziri huyo aliteuliwa mapema Septemba 2025, wakati ambapo nchi ilikuwa na hali ya machafuko ya umma na wasiwasi kuhusu usimamizi wa masuala ya taifa. Hali hiyo ilijiri baada ya serikali zilizopita kushindwa kupitisha bajeti zinazolenga upunguzaji wa matumizi na ongezeko la kodi, jambo lililokuwa limeibua utata mkubwa wa kisiasa.
Muda mfupi baada ya kujiuzulu kwake, Ikulu ya Ufaransa imetangaza kuwa Rais Emmanuel Macron amekubali barua ya kujiuzulu ya Lecornu, na sasa kuibuka maswali kuhusu nani atakayechukua nafasi yake na namna serikali itakavyoweza kurekebisha mgogoro wa bajeti na uhusiano na wawekezaji.