Waziri Mkuu wa Uganda, Robinah Nabbanja Atua Dar Kushiriki Mkutano wa Nishati

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda, Robinah Nabbanja, amewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, utakaofanyika leo tarehe 27 na 28 Januari 2025.
Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mheshimiwa Nabbanja amepokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Cosato Chumi.

Nabbanja yuko nchini kumuwakilisha Rais wa Uganda katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati ambao unawakutanisha Viongozi wa Afrika, wadau wa sekta ya nishati, na washirika wa maendeleo.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati unalenga kuimarisha juhudi za pamoja katika kukabiliana na changamoto za nishati barani Afrika na kuhakikisha nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu barani Afrika inapatikana kwa watu milioni 300 ifikapo mwaka 2030.


