Wizara Yakataa Ripoti Ya Wauguzi Waliozua Taharuki Baada Ya Video Yao Kusambaa – ”Sio Msimamo Wetu’

Hivi karibuni, Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) kilitoa maoni yake kuhusu tukio la video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua taharuki ikiwahusisha Bi. Rose Shirima (Muuguzi & Mkunga) na Bw. James G. Chuchu (Mteknolojia Maabara) watumishi wa Zahanati ya Ishihimulwa, Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora ambao walikuwa wakijibizana (bila staha) kuhusu matumizi ya kipimo cha haraka cha kupima malaria (MRDT) kinachodaiwa kuisha muda wake.
Maoni yaliyotolewa na TANNA tarehe 11 Januari, 2023 siyo msimamo wa Wizara ya Afya bali ni maoni yao kama chama hiari cha kitaaluma.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI inapenda kuwafahamisha umma kuwa zilituma timu ya watalaamu kuchunguza tukio hilo tangu lilipotokea na uchunguzi wa suala hili bado unaendelea. Mpaka sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Serikali.
Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI zitatoa taarifa rasmi kwa umma baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi. Wizara inawaomba wananchi kusubiri taarifa hiyo kutoka kwenye vyombo vyake.


