Yanga Bhana! Kama Mlivyosikia, Kocha Wao Afungua -Video

YANGA bhana! Kama mlivyosikia kwani imeshindwa kutamba kwa mara nyingine mbele ya Azam FC baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kwenye mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, jana huku mvua iliyonyesha ikitibua baadhi ya mipango ya kocha.
Hii inakuwa ni mechi ya pili kwa Kocha wa Yanga, Luc Eymael raia wa Ubelgiji kupokea kipigo baada ya awali kufungwa na Kagera Sugar mabao 3-0. Huku kile kipigo dhidi ya Mtibwa Sugar katika Mapinduzi alishuhudia akiwa jukwaani.

Kocha huyo ameanza wa rekodi mbovu ndani ya Yanga tofauti na kocha wa muda ambaye alikuwa akisimamia timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa.
Bao pekee la ushindi kwa Azam FC lilipachikwa dakika ya 25 na beki wa Yanga, Ally Mtoni ‘Sonso’ aliyejifunga akiwa kwenye harakati za kuokoa mpira uliopanguliwa na kipa Farouk Shikalo baada ya Azam kupiga kona kupitia kwa Bruce Kangwa.

Kwa matokeo hayo, Yanga imesalia katika nafasi ya nane, ikiwa na alama 25 ikicheza mechi 14, huku Azam ikipaa mpaka nafasi ya pili kwa kukusanya alama 32 nyuma ya vinara Simba wenye 38.

Mbelgiji huyo ameweka rekodi mbovu kwani ndani ya dakika 180 hajaambulia hata pointi moja chochote ndani ya kikosi hicho licha ya kufanya usajili wa nguvu kipindi cha dirisha dogo.
Yanga hivi sasa imeachwa pointi 13 na vinara Simba ambao leo Jumapili watacheza mechi yao ya 16 dhidi ya Alliance.

