Yanga Yaiwahi Medeama Ligi ya Mabingwa Afrika

MABOSI wa Yanga, wamepania timu yao kuvuna pointi tatu ugenini, watakapocheza dhidi ya Medeama FC, baada ya leo Jumaanne alfajiri kuamua kikosi hicho kuanza safari kuelekea nchini Ghana.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana katika mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaochezwa Desemba 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Baba Yara Sports uliopo Kumasi, Ghana.
Sio kawaida kwa Yanga, kusafiri kuwafuata wapinzani wao mapema kiasi hiki, lakini safari hii wanafasiri kwenda Ghana kuwafuata Medeama zikiwa zimebakia siku nne kabla ya mchezo huo.
Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kutoka ndani ya Kamati ya Utendaji ya Yanga, wameianza safari hiyo mapema ikiwa ni sehemu ya mikakati yao ya kupata muda mzuri wa kufanya maandalizi ya mchezo huo, ambao muhimu kwao kupata ushindi ugenini dhidi ya Medeama.

Alisema kuwa, kutua mapema huko Ghana, kutawapa muda mwingi wachezaji wao kupumzika, kwa ajili ya kupambana na kurejea nyumbani na ushindi ambao utafufumua matumaini ya kufuzu hatua inayofuatia.
Aliongeza kuwa, mchezo huo dhidi ya Medeama wanauchukulia kwa umuhikmu mkubwa, kwao kupata ushindi na siyo matokeo mengine.
“Kikosi chetu cha Yanga, kesho (leo Jumanne) kinatarajiwa kuondoka nchini, kuelekea Ghana tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Medeama ambao lazima tupate ushindi.

“Tumeianza safari hiyo mapema ikiwa ni mkakati wa kupata muda mzuri wa maandalizi na mapumziko ili kuwakabili wenyeji wetu kwa lengo la kupata ushindi ili kufufua matumaini ya safari ya kuelekea robo fainali.
“Iwapo tutafanikiwa kupata pointi hizo tatu ugenini, tutajiwekea mazingira mazuri ya kufuzu hatua inayofuatia ya michuano hii mikubwa Afrika,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia hilo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, alisema: “Kila mchezo uliopo mbele yetu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, tunauchukulia kwa umuhimu mkubwa ambapo unakwenda kurejesha matumain ya sisi kufuzu robo fainali.”

