
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi anatarajiwa kuhitimisha ziara yake ya kikazi katika Falme za Kiarabu (UAE) leo, Januari 19, 2022 huku tayari mafanikio makubwa yakiwa yameanza kuonekana kutokana na ziara hiyo.
Rais Mwinyi aliwasili Dubai Januari 17 na kuanza ziara hiyo ambapo mbali na mambo mengine, ameshuhudia utiaji wa saini wa miradi miwili mikubwa ya uwekezaji visiwani Zanzibar kati ya serikali na Mwekezaji wa Kampuni ya Eagle Hills Regionals Properties.
Pia, Rais Mwinyi amekutana na kufanya mazingumzo na Mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed Rashid Al-Makhtoum baada ya kumalizika kwa hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa shindano la Zayed Sustainability Prize Awards zilizofanyika Dubai.
Mtawala huyo ameahidi kujenga hoteli ya nyota tano katika eneo la Kizingo pamoja na nyumba za kisasa za makazi katika eneo la Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ajili ya soko la watalii na watu wenye uwezo.
Pia Rais Mwinyi amehudhuria katika maonesho ya kibiashara ya Dubai Expo 2020 na kutembelea Banda la Maonesho ya Tanzania pamoja na kukutana na kufanya mazungumzo na mwekezaji wa Kampuni ya International Holding (IHC).
Ziara hiyo inatajwa kuwa kichocheo kikubwa katika kuifungua Zanzibar kuelekea katika uchumi wa bluu, utakaoinufaisha serikali pamoja na wananchi wake.

