The House of Favourite Newspapers

BURUNDI YA NKURUNZIZA NI MFUPA ULIOMSHINDA MKAPA

KUONGEZA muda wa kutawala nchi kulii­fanya Burundi kuingia katika ghasia kubwa za kisiasa hata kuwepo kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi, hii ina maana kwamba wananchi wengi hawakuafiki jambo hilo.

 

Hata hivyo, serikali nchini humo inasema nchi imeshatulia na kurudi katika hali yake ya zamani. Na moja ya ziara yake nchini Tanzania mwaka jana, Rais Pierre Nkurun­ziza wa nchi hiyo, alimwambia Rais Dk. John Magufuli: “Burundi imekuwa na amani na utulivu,” huku mwenyeji wake akiwataka wananchi wa Burundi wabakie nchini mwao kwa kuwa ni shwari.

Lakini vikundi vinavyotetea haki za binadamu na wadadisi wa taasisi za kimataifa wanatoa picha tofauti kabisa. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliwahi kutoa ripoti kali inayoshutumu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini humo.

 

Mwezi Juni mwaka jana tume moja ya Umoja wa Mataifa ilisisi­tiza kuwepo kwa ukandamizwaji wa kutisha wa haki za binadamu na hali ya vitisho nchini humo kutoka vyombo vya dola.

Wakati huo huo ripoti nyingine iliyotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu (Federation for Human Rights- FIDH), ilidai kwamba mgogoro unaoendelea sasa hivi ume­sababisha vifo vya watu 1,200 na kutiwa kizuizini kwa wengine zaidi ya 10,000 kutokana na sababu za kisiasa.

Lakini kutofautiana huku kwa mitazamo kuhusu Burundi hakutokani na vita vya maneno, bali kunatokana na hatua zina­zotakiwa kuchukuliwa ili Burundi iondoke ilipo na isonge mbele.

 

Burundi ilitumbukia kwenye ghasia Aprili 2015 pale Rais Nkurunziza alipotangaza kugo­mbea urais kwa kipindi cha tatu kilichokuwa cha utata mkubwa. Maandamano yaliibuka pamoja na jaribio la kutaka kuipindua serikali yake likafanyika Mei 2015.

Pamoja na madai kwamba kipindi cha tatu kilikuwa kinyume na katiba, Julai mwaka huo, Nkurunziza aliendelea na azma yake ya kugombea urais na ikasemwa ameshinda.

Vurugu kubwa ziliibuka pamoja na mauaji ya watu mashuhuri. Maelfu ya watu waliyakimbia makazi yao, vyanzo vya upatikanaji habari viliminywa na wanahabari wa nchi za nje walitimuliwa.

 

Kutokana na hali hiyo, ma­shirika kadhaa ya kimataifa na ya kikanda yaliitaka Serikali ya Burundi na wapinzani kukaa meza moja kujadili matatizo yao.

Hata hivyo, mazungumzo rasmi hayajafanyika. Pamoja na duru kadhaa za majadiliano kutoka kwa wasuluhishi ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (ambayo Burundi ni mwana­chama) yalishindwa kushawishi serikali na wapinzani kukaa meza moja.

Chama Tawala cha CNDD-FDD, kinasisitiza hak­iwezi kuzungumza na wajumbe wa CNARED, chama kikuu cha upinzani kilicho uhamishoni, kwani kina­watuhumu kushiriki katika jaribio lile la mapinduzi.

 

Kiongozi wa majadiliano ya usuluhishi, rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, alisema Mei mwaka jana kuwa suala zima linakwenda polepole kwa sababu Serikali ya Burundi haitaki kukaa meza moja na wapinzani na wachambuzi wa­nalinganisha suala hilo na mfupa uliomshinda Mkapa.

Mazungumzo hayo yamekuwa yakiendelea kati ya serikali na makundi ya upinzani yalisam­baratika na Mzee Mkapa ali­yekuwa anafanikisha mazungum­zo hayo alisema hakukuwa na “makubaliano yoyote, maazimio yoyote au stakabadhi yoyote ya kuwafungamanisha wadau.”

 

Lakini Agosti mwaka jana ujumbe ulio karibu na serikali ulidaiwa kufanya mazungumzo ya siri na wawakilishi wa wapinzani ambao wako uhamishoni nchini Finland.

Hata hivyo, kuna baadhi wana matumaini kwamba habari hizi zinaashiria kufufuka kwa mazun­gumzo lakini Serikali ya Burundi iliamua kujiweka mbali na habari zenyewe.

Itaendelea wiki ijayo.

Elvan Stambuli na Mitandao

Mambosasa: Abdul Nondo Alikwenda Iringa kwa Mpenzi Wake

Global Publishers and General Enterprises Limited is a registered private company dealing in publishing of weekly Swahili newspapers in Tanzania, namely; Uwazi, Ijumaa, Championi, Amani, Risasi & Ijumaa Wikienda.

You might also like More from author

Comments are closed.