The House of Favourite Newspapers

Mfalme wa Morocco Kuwasili Nchini Keshokutwa

makonda
MFALME Mohamed VI wa Morocco anatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa Oktoba 23 ambapo atapokelewa na Rais John Magufuli.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (pichani juu), amesema kuwa mfalme huyo anatarajiwa kuwasili hapa nchini majira ya saa kumi jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere katika ziara ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili.

Amesema baada ya kutua uwanjani hapo atakagua gwaride maalum na baadaye ataelekea sehemu atakayokuwa amepangiwa kufikia.
Kiongozi huyo atakuja na msafara mkubwa wa ndege sita ambazo zitakuwa na viongozi na wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo watalii.

Makonda amewaomba wananchi radhi kwa usumbufu utakaojitokeza kwani barabara itakayotumika kwa msafara wa magari kumpokea mgeni huyo ni barabara za Nyerere, Gerezani na Sokoine.

Alifafanua kwamba ujio wa mfalme huyo utaiwezesha Tanzania kupata fursa mbalimbali ya kuzungumza na kubadilishana mawazo juu ya fursa za kibiashara zinazopatikana hapa nchini ili kuongeza wigo wa kibiashara.
Mgeni huyo anatarajiwa kuondoka nchini Oktoba 27.

Na Denis Mtima/Gpl

Comments are closed.