The House of Favourite Newspapers

Wasiohakiki TIN Dar Watakiwa Kwenda Mamlaka ya Mapato

Kutoka kushoto ni Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mariam  Mwayela, Richard Kayombo na Ofisa Mwandamizi wa Mahusiano ya Jamii, Regnihaldah Mpete.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo, akizungumza na wanahabari.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wakazi wa Dar es Salaam ambao hawakuhakiki Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) katika mchakato ulioanza Agosti 16, mwaka jana na kuhitimishwa Januari 31, mwaka huu waende kwenye ofisi za mamlaka  hiyo katika mikoa yao ya kodi kwa maelekezo.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam,  Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo,  amesema zoezi hilo kwa upande mmoja lilienda vizuri kutokana na ushirikiano wa wananchi walioutoa wakati wa zoezi hilo.

Hata hivyo, alisema, kutokana na sababu mbalimbali imebainika kwamba baadhi ya wananchi walishindwa kukamilisha zoezi hilo katika muda uliopangwa na hivyo wametakiwa kulikamilisha.

Alisema kwa wananchi waliokuwa nje ya nchi kwa sababu mbalimbali katika kipindi cha uhakiki watafanya uhakiki pindi watakaporudi nchini kwa kuonyesha vielelezo vya kuthibitisha wao kutokuwepo nchini.

“Baada ya kumaliza awamu ya kwanza ya uhakiki kwa Mkoa wa Dar es Salaam, mamlaka itaendelea na awamu ya pili katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Morogoro, Tanga, na Pwani. Zoezi litaanza rasmi Februari 15  mwaka huu na kumalizika Machi 31 mwaka huu na tarehe ya kutangazwa mikoa iliyobaki tutaitangaza baadaye.

“Pia kwa watakaobainika kuwa na TIN zaidi ya moja, utaratibu uliopo ni wa kuhuisha taarifa ya mojawapo ya TIN hizo na kuzifunga nyinginezo. Endapo mtu ana madeni ya kodi katika mojawapo ya TIN hizo au zaidi, utaratibu wa kudai madeni utaendelea kwa mujibu wa sheria na mamlaka haitamzuia mwenye deni kuhakiki TIN yake,” aliongeza.

Alisema kuwa kwa ufafanuzi zaidi wananchi wanaweza kuwasiliana na kituo cha huduma kwa walipakodi kwa kupiga simu za bure namba 0800750075/0800780078 au Barua pepe huduma @tra.go.tz

Na Denis Mtima/GPL

Save

Comments are closed.