The House of Favourite Newspapers

Unaumia Wakati wa Tendo la Ndoa? Soma Hapa!

HII ni hali ambayo mwanamke anakuwa na hamu ya kufanya tendo  la ndoa lakini anapata ugumu kutokana na maumivu makali anayopata.

Hali hii inatokana na kubana au kukaza kwa misuli ya uke lakini pia  inaweza kusababishwa na matatizo ukeni.

Mfano endapo kuna michubuko au vidonda au kasoro yoyote ya uke,  aidha uke ni mdogo au maumbile ya uke hayana uwiano na uume. Tatizo hili huwapata wanawake wa rika zote ilimradi tayari yupo katika  umri wa kuzaa.

TATIZO LINAVYOGAWANYIKA

Tatizo hili la maumivu wakati wa tendo la ndoa limegawanyika katika maeneo makuu mawili. Kwanza ni Primary Dyspareunia .

Hapa  mwanamke anakuwa hana historia ya maumivu wala  hana historia ya kuwahi kufanya tendo hilo ndiyo, kwanza anaanza. Kitaalamu hali hii ya maumivu huitwa Honey moon Dypareunia au maumivu ya fungate na hutokea mara tu anapoanza kujamiiana kwa mara ya kwanza. Katika hali hii misuli ya uke inaweza kubana kutokana na michubuko au kuchanika ubikira au hata kuchanika upande wa chini wa uke na wakati mwingine  michubuko hutokea katika tundu ya mkojo.Hali ya michubuko inaweza kuwa mbaya na ikajitokeza hata kwa kugusa tu upande wa nje wa uke.

Maumivu yakiendelea au yakizidi husababisha mgonjwa apate matatizo ya kisaikolojia kiasi kwamba huanza kuogopa tendo lenyewe na kuhisi endapo atalifanya ataumia. Tatizo hili likileta michubuko kwenye njia ya mkojo husababisha maambukizi sugu ya kibofu cha mkojo kutokana na michubuko ya mara kwa mara ya tundu ya mkojo.

Maumivu ukeni hutokana pia na maandalizi mabovu kabla ya tendo ambapo uke unakuwa haujalainika kwa kutofanya romance ya kutosha,  kutofanya tendo hilo kwa ustaarabu, yaani kutumia nguvu au endapo mwanamke atakuwa na maambukizi ukeni mfano fangasi ambayo huambatana na kutokwa na uchafu ukeni na muwasho, magonjwa ya uke kama kuvimba kwa tezi za uke, kuvimba kwa mashavu ya uke au hali yoyote inayomwondolea amani mwanamke pale ukeni inaweza kumfanya kisaikolojia aathirike na kuhisi maumivu wakati wa tendo.

Michubuko ukeni au kuhisi moto ukeni wakati wa tendo la ndoa kunaweza kusababishwa na matumizi ya vilainishi visivyofaa  au kuumwa kutokana na uwepo wa vinyweleo virefu ukeni na endapo havikupunguzwa vitaingia ukeni wakati wa tendo na kukuchubua.  Kasoro katika ubikira pia husababisha mwanamke ahisi maumivu wakati wa tendo.

Maumivu haya huwa hayahusiani na yale ya awali ya fungate na wakati mwingine huanza baada ya kipindi kirefu cha miaka
mingi tangu uanze tendo la ndoa na wengine huwa na tatizo hili tayari wana watoto. Chanzo cha tatizo hili ni ukavu ukeni, umri mkubwa wa mwanamke na kusinyaa kwa misuli ya uke.

Matatizo haya isipokuwa la umri mkubwa  hutokea katika umri wa kati na tayari mwanamke  anayo historia ya kuwa katika mahusiano na hata tayari ana watoto. Umri mkubwa tunaouzungumzia ni zaidi ya miaka hamsini. Kubana misuli ya ukeni hutokana na makovu baada ya kushonwa msamba au kuongezewa njia wakati wa kujifungua au upasuaji wa kurekebisha fistula pia husababisha tatizo hili.

Vyanzo vingine vya maumivu haya ya tendo la ndoa ni kushuka kwa kizazi ambapo mwanamke atahisi kitu kama gololi ukeni wakati  akijisafi sha au kuhisi kizazi kinasukumwa wakati wa tendo, kugeuka kwa kizazi, matatizo katika tabaka la ndani la kizazi, maambukizi sugu ukeni ambapo uchafu na muwasho ukeni hujirudiarudia, matatizo katika njia ya mkojo na maambukizi katika viungo vya uzazi ’PID’  husababisha maumivu wakati wa tendo la ndoa.

Matitizo ya kisaikolojia husababisha maumivu wakati wa tendo la ndoa pale ambapo misuli ya ukeni itakaza na mwanamke anapochunguzwa huwa hana tatizo au kasoro yoyote ukeni. Matatizo katika mishipa ya fahamu ya ukeni, kuogopa tendo lenyewe kuhisi utapata maumivu au kama kuna historia ya kuingiliwa kwa nguvu na ukaumia, kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu tendo la kujamiiana, yote haya na mengine mengi humharibu mwanamke kisaikolojia na kujikuta anaanza kuhisi maumivu hata kabla ya tendo lenyewe kwa kuingiwa na hofu.

Hali nyingine inayoweza kumfanya mwanamke aathirike kisaikolojia na asiwe tayari kwa tendo na hata akilifanya apate maumivu ni kuogopa kupata ujauzito wakati hayupo tayari kwa hilo, kuogopa kupata maambukizi, kulazimishwa penzi endapo haupo tayari na mwanaume uliye naye na kuhisi kuna tofauti ya maumbile na mume uliyenaye.

Endapo mwanaume anakukwaza kutokana na kutokwa na jasho jingi sana wakati wa tendo, kutoa harufu mbaya ya pua, kinywani, makwapani au sehemu zake za siri, huwa na magonjwa ya ngozi au hata mwilini mwake, matatizo haya huweza kumwathiri mwanamke kisaikolojia na asifurahie tendo na kutotoa ushirikiano wakati wa tendo na kupata maumivu.

UCHUNGUZI Tatizo hili ni pana sana, unaweza kuhisi una kasoro au maambukizi kumbe tofauti. Kwa hiyo basi ni vizuri uchunguzwe kwa umakini katika kliniki za madaktari wa akina mama katika hospitali za mikoa ili kujua chanzo halisi cha tatizo.

Comments are closed.