The House of Favourite Newspapers

Faiza Ally: Acha Ulimbukeni, Unawadhalilisha Wenzio

Faiza Ally.

 

SARAKASI za Faiza Ally kwenye mitandao ya kijamii zinachosha! Zinachefua! Zinatia aibu… kuna wakati unajiuliza mara mbilimbili, matendo yake huwa yanachochewa na nini?

 

Ni akili za kitoto? Hapana, Faiza hana utoto wowote. Anatumia madawa? Watu wake wa karibu wanamtetea kwamba hatumii hizo mambo. Anafanya makusudi? Yawezekana ikawa ni kweli lakini malengo ya kufanya makusudi yanayoudhalilisha utu wake ni nini? Anatafuta kiki? Ili iweje?

 

Mlolongo wa maswali unayoweza kujiuliza utakapoanza kukisumbua kichwa chako kumtafakari Faiza Ally ni mrefu, tena mrefu haswaa! Kwa wasiomfahamu, huyu ni msanii wa filamu za Kibongo ambaye kuna wakati aliwahi kufanya poa ingawa siyo kivile kwenye filamu lakini pia ni mjasiriamali!

Kama utambulisho huo haujatosha, basi huyu ndiye mzazi mwenzake Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, bila shaka sasa unaelewa namzungumzia nani. Kwa kumtazama, ni mpole, mkimya na yupo ‘natural’ f’lani hivi! Kama humjui unaweza kumpenda bure, hasa ukipata nafasi ya kumtazama na kumsikiliza anapoongea ana kwa ana.

 

Kilichojificha nyuma ya mwonekano wake wa nje usio na hatia, ni kwamba kuna kitu hakipo sawa kwenye akili yake, mshipa wake wa aibu ulishakatika, tena kitambo tu. Anafanya mambo ambayo wakati mwingine usipopewa ushahidi unaweza kumtetea kwamba anasingiziwa!

 

Tukio linalotingisha mitandaoni kwa sasa, ni kitendo chake cha kujirekodi video akiwa ameshika nguo ya ndani (kufuli) iliyochoka, huku akiitolea ufafanuzi kwa nini ameendelea kuitunza kwa miaka kibao licha ya kwamba imetobokatoboka na kufubaa.

 

Ni jambo linalotia aibu sana kuona mwanamke, tena kioo cha jamii anakuwa mstari wa mbele kufanya mambo ya ajabuajabu yanayoudhalilisha utu wa mwanamke, tena hadharani! Anataka watoto na wadogo zetu wa kike waliopo mashuleni wajifunze nini kupitia huo ujinga wake?

 

Ipo haja sasa kwa mamlaka zinazohusika kumtazama kwa sababu ipo siku atafanya jambo litakalochafua kabisa hali ya hewa kwa sababu hii si mara yake ya kwanza. Drama za Faiza zilianza kitambo, pale alipovaa ‘pampas’ kwenye siku yake ya kuzaliwa, akaja tena kutibua hali ya hewa pale kwenye Sherehe ya Zari All White Party akiwa ametinga shati tu na kufuli bila kujistiri na sketi au suruali kama wanawake wenzake wanavyofanya. Yaani alivaa shati tu, hebu vuta picha!

 

Akaja kutia tena aibu kwenye sherehe za utoaji wa Tuzo za KTMA mwaka 2014, pale alipotinga ‘red carpet’ akiwa na kivazi kilichoyaacha makalio yake nje kiasi cha kuwafanya watu wazibe midomo kwa mshangao.

Yote tisa, kumi ni hapa juzikati alipopost kwenye akaunti yake ya Instagram picha yake akiwa anajifungua! Kwa waliobahatika kuiona picha hii watakuwa wananielewa ninachozungumza!

 

Sote tunayajua maumivu na mateso waliyoyapata au wanayoendelea kuyapata mama zetu, wake zetu na dada zetu wanapojifungua, ukiwasikia tu wanavyosimulia shughuli inavyokuwa pevu ‘leba’, hakika unawaonea huruma.

Hospitali nyingi, wanaume hawaruhusiwi kabisa kusogelea ‘leba’ isipokuwa madaktari wenyewe au mume wa mwanamke husika pale inapolazimu kufanya hivyo, sote ni mashahidi kwamba hakuna kitendo kinachoheshimika kama kujifungua.

Sasa mwanamke anapopost picha akiwa utupu akijifungua, kama si kuwadhalilisha wanawake wenzake ni nini? Lengo lake lilikuwa ni kuonesha nini?

Au kwa sababu Wazungu huwa wanajirekodi video wakiwa leba basi na sisi kila kitu tunaiga bila kutazama mila na tamaduni zetu zinasemaje? Unaweza kujiuliza maswali mengi yasiyo na majibu kuhusu huyu Faiza.

 

Ni picha ambayo huwezi kuitazama mara mbili, kwa kifupi ni udhalilishaji wa wanawake uliovuka kiwango.

Kibaya ni kwamba mitandao ya kijamii, kila mtu mwenye simu anaweza kuingia na kuona uchafu huo, si mkubwa si mtoto, si mwanaume wala mwanamke, si mwanafunzi wala mkulima!

Unajaribu kuvuta picha, miaka michache ijayo mwanaye atakapopevuka kiakili, atakapokuwa na uwezo wa kuona picha alizoposti mama yake, atakuwa na nini cha kujivunia mbele za wenzake?

 

Huwezi kupata majibu kuhusu utendaji wa kichwa ya mwanadada huyu na zaidi utachoka pale anapojitetea ‘as if’ hakuna chochote kibaya alichokifanya. Unaweza kujiuliza mara mbilimbili, familia yake inajisikiaje kwa haya anayoyafanya?

Watu wake wa karibu wanajisikiaje? Mzazi mwenzake ambaye ni mtu maarufu kwenye siasa na muziki, japokuwa hawapo pamoja anajisikiaje kumuona mama wa mwanaye akifanya mambo yasiyopaswa kufanywa hata na binti anayeanza kuvunja ungo?

Faiza, ushakuwa mtu mzima sasa, acha ulimbukeni, unawadhalilisha wanawake wenzako. Jipange kabla mamlaka husika hazijakupanga.

Comments are closed.