
MSHAMBULIAJI bora wa PSG Neymar Santos Junior, huenda akakosekana katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya timu yake ya zamani Barcelona, unaotarajiwa kufanyika jumanne ijayo ya tarehe 16/02/2021.
Neymar aliumia katika mchezo wao wa kombe la Ufaransa ‘France Cup’ walipokuwa wanacheza na Caen, na alilazimika kutolewa na machela hali iliyoleta hofu zaidi kwa mashabiki kuwa huenda wakamkosa kwa muda mrefu, licha ya mchezo kumalizika kwa PSG kuibuka na ushindi wa 1-0 goli lililifungwa na Moise Kean.
Kocha wa PSG Mauricio Pochettino alisema; ”Siwezi kujutia kumtumia katika mchezo huu licha ya kutambua kuna mchezo mkubwa mbeleni dhidi ya Barcelona,Neymar alikuwa tayari kuitumikia timu yake kama ambavyo ingetokea kwa mchezaji yoyote.”
Neymar alihamia PSG mwaka 2017 akitokea Barcelona kwa ada ya uhamisho iliyovunja rekodi ya duniani ya yuro milioni 222 iliyozua tafrani baina ya timu hizo mbili,hadi bodi ya ligi ya ‘la liga’kuingilia kati chini ya Javier Tabes na kupata muafaka.
Neymar Santos Junior yupo katika kiwango bora sana kwa sasa amefunga magoli 6 katika michezo 11 ya ligi na kumfanya afikishe magoli 83 katika michezo 102 aliyoichezea PSG tangu ajiunge nayo 2017, ambapo mtizamo wa wengi unaonyesha endapo atakosekana timu itapungua ubora.

