Watu 50 Wameuawa Nchini Burkina Faso Baada ya Kuvamiwa na Waasi

WATU wasiopungua 50 wamefariki katika shambulio kwenye kijiji kimoja Kaskazini mwa nchi ya Burkina Faso, taarifa hiyo imethibitishwa na Msemaji wa Serikali.
Shambulizi hilo limetekelezwa na wavamizi hao usiku wa jumamosi na jumapili katika mji wa Seytenga sehemu ya jimbo la Seno ambalo lipo katikati ya mpaka ambao wapiganaji wa Al- Qaeda na ISIS wanatekeleza mapigano.

“Hadi sasa jeshi limekusanya zaidi ya miili 50, baada ya kijiji cha Seytenga kuvamiwa usiku wa jumamosi.” Alisema msemaji Lionel Bilgo huku akibainisha kuwa idadi inaweza kuongezeka.
Kumekuwa na mkanganyiko wa taarifa juu ya idadi ya vifo ambapo Afisa Usalama aliliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa watu 100 waliripotiwa kufariki, huku chanzo kingine cha cha habari kutoka ndani ya eneo hilo ambacho hakikutaka kuwekwa wazi kilibainisha kuwa zaidi ya watu 165 walifariki katika shambulio hilo.

Tayari Umoja wa Mataifa umelaani shambulio hilo kwa kudai limechukua maisha ya watu wasio na hatia, huku ukitaka Serikali na Mamlaka husika kuwakamata wahusika na sheria ichukue mkondo wake.
Umoja wa Ulaya nao umekemea shambulio hilo kwa kudai kuwa kuna haja kusimamisha mauaji hayo.

“ Njia zinazotumika na magaidi za kushambulia kila kinachoonekana mbele yao ni jambo la kukemewa.” alisema Mkuu wa sera za kimataifa kutoka Umoja wa Ulaya Josep Borrell.
Seytenga ilikuwa ni eneo la mapigano wiki iliyopita kati ya vikosi vya Serikali na vya waasi ambapo askari 11 walifariki na kusababisha oparesheni maalum ya majeshi ya Serikali ambapo iliripotiwa waasi 40 kuuawa.

