Serikali ya Kijeshi Burkina Faso Yafuta Vyama Vyote vya Siasa

Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imefuta vyama vyote vya siasa na kubatilisha mfumo wa kisheria uliokuwa unasimamia uendeshaji wake, kufuatia amri iliyoidhinishwa na Baraza la Mawaziri la nchi hiyo siku ya Alhamisi.
Hatua hiyo imechukuliwa chini ya utawala wa kijeshi unaoongozwa na Rais Ibrahim Traoré, aliyeingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi ya Septemba 2022, na inaelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha udhibiti wa mamlaka na kuijenga upya dola baada ya kusimamishwa kwa shughuli zote za kisiasa mara baada ya mapinduzi hayo.
Akizungumza baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burkina Faso, Emile Zerbo, alisema uamuzi wa kufuta vyama vya siasa unatokana na tathmini ya kina iliyofanywa na serikali, ambayo ilibaini kuwa mfumo wa vyama vingi ulikuwa unatumika vibaya na kushindwa kutimiza malengo yake ya msingi.
Zerbo alisema kuongezeka kwa idadi ya vyama vya siasa nchini humo kulichangia migawanyiko ya kijamii na kisiasa, hali iliyodhoofisha mshikamano wa kitaifa katika kipindi ambacho taifa hilo linakabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama.
Kabla ya mapinduzi ya kijeshi, Burkina Faso ilikuwa na zaidi ya vyama vya siasa 100 vilivyosajiliwa rasmi, huku takribani vyama 15 vikiwa na uwakilishi katika Bunge la Taifa kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Kwa mujibu wa amri hiyo mpya, vyama vyote vya siasa na miungano ya kisiasa vimevunjwa rasmi. Aidha, sheria inayobatilisha kanuni zilizokuwa zinasimamia usajili wa vyama, ufadhili wake pamoja na hadhi ya kiongozi wa upinzani, inatarajiwa kuwasilishwa katika Baraza la Mpito kwa ajili ya kuidhinishwa.
Serikali pia imetangaza kuwa mali zote za vyama vya siasa vilivyovunjwa au kufutwa zitahamishiwa mikononi mwa dola, hatua inayotarajiwa kuzua mjadala mpana ndani na nje ya nchi kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini Burkina Faso.
Burkina Faso, taifa la ukanda wa Sahel, limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya makundi ya wanamgambo wa Kiislamu yanayohusishwa na al-Qaeda na Islamic State. Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya raia na kusababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.
Hatua ya kufutwa kwa vyama vya siasa inaifanya Burkina Faso kuendelea kufuata mkondo unaofanana na nchi jirani za Mali na Niger, ambazo pia ziko chini ya tawala za kijeshi zilizochukua madaraka kupitia mapinduzi, huku wakisisitiza kuwa usalama wa taifa na uthabiti wa dola ni vipaumbele vyao vikuu.

