The House of Favourite Newspapers

Yanga na Singida Lazima Mmoja Afungwe Leo

Kikosi cha timu ya Yanga

 

SINGIDA na Yanga zimewahi kukutana mara tatu, kwenye mashindano tofauti zikaishia kuchekeana chekeana na kugawana pointi. Lakini kwa leo Jumapili ni shughuli tofauti kabisa kwani lazima mmoja afundishwe umuhimu wa matokeo.

 

Hakutakuwa na uswahiba baina na wachezaji au kati ya kocha na wachezaji wake wa zamani. Yaani liwake jua au inyeshe nvua lazima mtu afungwe kwenye mchezo huo wa robo fainali ya Kombe la FA, itakayopigwa ndani ya Uwanja wa Namfua.

 

Yanga inapiga hesabu ngumu za mechi tatu za FA ikiwemo ya leo ili kutafuta nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani, huku Singida na wenyewe wakipambana kuweka rekodi kutokana na uwekezaji waliofanya msimu huu.

 

Timu zote mbili zinautolea macho mchezo huo kwavile kwenye ligi kuu ushindani ni mkubwa zaidi huku hesabu za ubingwa zikigoma kuipa matumaini Singida ya Kocha mzoefu,Hans Pluijm.

Yanga leo itamrejesha uwanjani japo kwa dakika chache akiingia kutoka benchi straika wake aliyekuwa majeruhi, Donald Ngoma ambaye alisajiliwa Yanga ya Pluijm enzi akiwa Jangwani kama kocha.

Lakini Singida ambao wanacheza soka la kuvutia kutokana na usajili wa

 

 

kisomi, itamkosa straika wake, Danny Usengimana ambaye ametimkia kwao Rwanda kwa madai kwamba hajamaliziwa dau lake la usajili huku habari zikidai kuwa ameanza mazungumzo na timu moja ya Dar es Salaam.

Wachezaji wa timu ya Singida.

Yanga ambayo inakabiliwa na mechi ya mtoano ya Kombe la Shirikisho wikiendi ijayo dhidi ya Wolayta Dicha ya Ethiopia Jijini Dar es Salaam, inazipigia hesabu kali dakika 270 ambazo ni mechi tatu za kombe la FA hadi fainali.

 

Rekodi zinaonyesha kuwa hii itakuwa ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana katika uwanja huo baada ya awali kukutana Novemba 4, 2017, ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara uliomalizika kwa suluhu.

Nje ya ligi kuu, kwa msimu huu wamekutana tena katika Kombe la Mapinduzi ambapo Singida ilishiriki kwa mara ya kwanza na matokeo yakawa sare ya bao 1-1.

 

Tshishimbi ambaye si mzungumzaji sana alipoulizwa kuhusiana na mchezo huo alijibu kwa kifupi; “Kikubwa tunamuomba Mungu tuweze kufanya vizuri kwenye michezo yetu yote iliyosalia kwenye michuano tunayoshiriki, tumejiandaa vizuri kufanya hivyo ingawa tuna michezo migumu.”

 

Kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa ‘Fusso’, amesema: “Tunaingia kwa tahadhari kwani huu si mchezo rahisi, kikosi kiko vizuri, zaidi tunahitaji kusonga mbele.”

 

Kocha wa Singida United, Hans van Der Pluijm raia wa Uholanzi, amesema: “Tumejipanga na nimekuwa nikikinoa kikosi changu hasa safu ya ushambuliaji ili tufunge mabao na kumaliza kazi ndani ya dakika 90.”

 

Mkurugenzi wa Singida, Festo Sanga, amesema: “Hatujawaahidi wachezaji lolote zaidi ni kupata ushindi na ndiyo maana tuliweka kambi nje ya mji ili kupata utulivu.”

 

Yanga kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Hussein Nyika, alisema; “Tumejiandaa kupambana ndiyo maana kocha alipendekeza kambi Morogoro kwa sababu timu ilipotoka Botswana ilipata mapumziko kidogo na hali ya pale haina tofauti na Singida.”

Comments are closed.