The House of Favourite Newspapers

Yanga Mmejifunza Hatutaki Kuwaona Mkirudia Makosa

Kikosi cha timu ya Yanga.

YANGA wikiendi hii inatarajiwa kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikivaana na Wolayta Dicha ya nchini Ethiopia mchezo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa.

 

Yanga wanakutana na Waethiopia baada ya Caf kuchezesha droo na kujikuta timu hiyo ikiangukia kwa Dicha timu ambayo ilikuwa mabingwa wa Kombe la FA Ethiopia.

 

Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa Yanga kuwakaribisha wapinzani wao hao kabla ya kurudiana wiki moja baadaye.

Ikumbukwe kuwa, Yanga inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa na Township Rollers ya Botswana siku chache zilizopita.

 

Nirudi kwenye mada yangu ya leo na kikubwa nilikuwa nawatahadharisha Yanga kutorudia makosa waliyoyafanya kwenye Ligi ya Mabingwa na y a l i y o w a s a b a b i s h i a waondolewe na kuangukia katika Kombe la Shirikisho.

Yanga katika michuano hiyo imekuwa ikifanya makosa yaleyale kila mwaka wanaoshiriki michuano ya kimataifa na kikubwa wanashiriki bila ya malengo nikimaanisha mbinu thabiti zitakayowawezesha wao kufika mbali na badala yake kujikuta ikitolewa katika hatua ya mtoano.

 

Mbinu hizo ni kushindwa kutumia vema uwanja wa nyumbani, hilo ni tatizo sugu kwa Yanga mara kadhaa imekuwa ikipata matokeo mabaya nyumbani lakini katika michezo ya marudiano ya ugenini inapata mazuri na zaidi inacheza kwa kiwango kikubwa.

Hapo, utaona utofauti mkubwa kati ya Simba na timu nyingine zenye uzoefu wa kushiriki michuano hiyo mikubwa ambazo zenyewe hazikubali kupoteza mchezo wa nyumbani.

 

Yanga sasa mnaendelea katika michuano hiyo mikubwa ya Afrika ninaamini mmejifunza sasa kipi mkifanye ili muwaondoe Waethiopia katika mechi hii ya kwanza mtakayoicheza Jumamosi wiki hii.

Kwani timu ikipata ushindi mzuri wa nyumbani inapunguza presha ya mechi ijayo ya marudiano ambayo itakuwa ugenini ikiwemo kucheza kwa kujiamini.

 

Na kingine itawasaidia kukwepa hujuma za wapinzani wao, kama unavyofahamu michuano hii mikubwa inakuwa na michezo mingi michafu ya ndani na nje ya uwanja, hivyo basi kwa kutumia mbinu hiyo ya ushindi wa nyumbani itawasaidia kukwepa hujuma hizo.

 

Mfano mzuri, Simba walipokwenda kurudiana na Al Masry walikutana na matukio mengi ya nje ya uwanja kwa maana ya basi lililoandaliwa na wapinzani wao Al Masry kwa ajili ya kuwapokea wachezaji na kuwapeleka hotelini lilikutwa lina harufu ya tofauti ambayo kwa mujibu wa uongozi wa Simba, lilipuliziwa dawa ‘spray’.

 

Tofauti na tukio lingine ni lile la viongozi wa Misri kuwaweka mashabiki wa Simba kwenye jukwaa ambalo lipo mbali na ‘pitch’ kwa makusudi ili mashabiki wasisikike wakiwasapoti wachezaji hao kwa makusudi, hiyo ni moja ya hujuma za wapinzani.

Ni muda muafaka wa viongozi na benchi ya ufundi ya timu hiyo chini ya Kocha Mkuu Mzambia, George Lwandamina kujifunza na kushika mbinu hizo nilizowapa za kutumia vema uwanja wa nyumbani katika mechi zake za kimataifa.

 

Yanga waliangalie hili nalo la kucheza kwa tahadhari kwa maana ya kulinda na kushambulia lango la wapinzani katika mechi hiyo ya nyumbani kwani wakiwa nyumbani wakiruhusu bao moja ni faida kubwa kwa wapinzani kwani wanapata bao la ugenini.

Kwani Yanga ikiwa nyumbani na kujisahau na kushambulia lango la wapinzani muda wote bila kulinda lango lao itawafanya waruhusu bao langoni kwao na kujiwekea mazingira mabaya ya bao la ugenini.

 

Hivyo, kitu wanachotakiwa kukifanya ni kulinda lango lao na kufanya mashambulizi ya kushitukiza ndani ya wakati ambayo ndiyo mbinu sahihihi kitu ambacho Yanga walishindwa kukifanya na kusababisha kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa.

Kitu kingine ninachowatahadhar i sha Yanga ni nidhamu ya uwanjani kwa maana ya wachezaji kucheza kwa tahadhari ili kuepuka kadi za njano na nyekundu zisizokuwa na ulazima kuepuka kuikosa michezo ijayo.

MAKALA: JOHN JOSEPH

Comments are closed.