The House of Favourite Newspapers

Yanga Lazima Washinde Leo Dhidi Ya Wolayta Dicha Ya Ethiopia

YANGA itawakosa nyota wanne wa kikosi cha kwanza pia makocha wake wasaidizi hawatakuwa benchi kutumikia adhabu za Shirikisho la Soka Afrika (Caf), ila wenyewe wamesisitiza lazima washinde leo dhidi ya Wolayta Dicha ya Ethiopia.

 

Leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga itaikaribisha Dicha kucheza mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho.

 

Yanga itawakosa nyota wake Papy Kabamba Tshishimbi, Said Makapu, Obrey Chirwa na Kelvin Yondani wenye kadi mbili katika michuano hiyo huku makocha wake wasaidizi Noel Mwandila na Shadrack Nsajigwa wakielekezwa kukaa jukwaani.

Caf iliitumia Yanga taarifa ya wachezaji hao kutotakiwa kucheza kutokana na kadi mbili walizonazo lakini kwa Yondani, timu hiyo ilikana kwamba hana kadi mbili za njano. Shirikisho hilo pia liliiambia Yanga kuwa, kocha wake msaidizi Mwandila hatakiwi kukaa benchi kwani alitolewa katika mchezo wa marudiano dhidi ya Township Rollers nchini Botswana.

 

Usahihi ni kwamba, aliyetolewa ni Nsajigwa hivyo Yanga imeamua wote wawili hawatakuwepo katika benchi ili kuepuka adhabu isiyo ya lazima kwao. Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa aliliambia Championi Jumamosi kuwa, pamoja na mambo yote hayo wao watapambana ili kushinda mechi hiyo ya kufuzu makundi Kombe la Shirikisho.

Papy Kabamba Tshishimbi atacheza leo kutokana na kadi mbili za njano.

“Pamoja na mambo yote hayo, sisi tumesimama imara kushinda mechi hii, pia hatutajali kwani wapinzani wetu waliwatoa Zamalek na Zimamoto (ya Zanzibar), kwani nasi tunataka kwenda mbele. “Tumeuona mfumo wao na sisi tumebadili wetu kidogo na tutawazuia muda wote huku tukiwashambulia kadiri tunavyopata nafasi, tunajua ni wazuri katikati sasa sisi tutapitia pembeni kuwashambulia.

 

“Tumefika leo (jana) asubuhi kutoka Morogoro tulipoweka kambi ya siku nne, tupo vizuri na hata zile nafasi za wachezaji ambao hawatacheza tumezipatia watu wengine. “Hawa wapinzani wetu tutawafunga sababu watajiamini kupita kiasi sababu waliitoa Zamalek ya Misri katika mechi ya hatua iliyopita, hivyo tumejiandaa kuwatoa,” alisema Nsajigwa.

MZIKI UMETIMIA N

sajigwa alisema kutokana na kuwakosa Tshishimbi, Chirwa, Yondani na Makapu wenye kadi mbili za njano, nafasi zao watacheza Shaibu Ramadhan ‘Ninja’, Pato Ngonyani, Thabani Kamusoko na Yohana Nkomola. Hii inamanisha kwamba, nafasi ya Yondani atacheza Ninja, nafasi ya Makapu atacheza Pato, nafasi ya Tshishimbi atacheza Kamusoko na nafasi ya Chirwa atacheza Nkomola.

 

“Tunaamini wachezaji hao watacheza vizuri kama ambavyo wangekuwepo hawa ambao hawapo, tunaamini kila mchezaji ndiyo maana tuliwasajili,” alisema Nsajigwa. Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, alisema; “Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hii na ni matumaini yangu kuwa tushinda.”

 

BOSSOU AUZA SIRI ZA YANGA Beki wa zamani wa Yanga, Vincent Bossou ametajwa kutoa siri za Yanga kwa nahodha wa Dicha, Djako Arafat ambaye straika ni raia wa Togo kama ilivyo kwa Bossou.
Arafat aliliambia Championi Jumamosi kuwa; “Naifahamu vizuri Yanga, niliifuatilia katika mitandao halafu kaka yangu Bossou ameniambia kila kitu kuhusu Yanga.

 

“Bossou ameniambia amewahi kucheza hapa na ametaja ubora na udhaifu wa mabeki wa Yanga, hivyo hii ni mechi ngumu na nimewaambia wenzangu tupambane ili tukamalize kazi nyumbani.” Mkuu wa Ufundi wa Dicha, Habtom Hailemichael alisema: “Sifahamu Yanga, sijaiona popote sisi tutacheza kwa mfumo wetu ambao hautabadilika.” Hailemichael alisema anasikitika kumkosa straika Teklu Tafese Kumma ambaye ana adhabu ya kadi mbili za njano katika michuano hiyo.

YANGA IKISHINDA MAMILIONI MLANGONI

Kama Yanga ikishinda mechi ya leo, itajiweka karibu na kufuzu hatua ya makundi ambayo kila timu hupewa dola 150,000 sawa na Sh milioni 337.5. Ushindi wowote ule utaipa nafasi Yanga ya kukomaa katika mechi ya marudiano nchini Ethiopia hata kupata sare na kufuzu hatua ya makundi.

 

NGOMA, TAMBWE NDIYO BASI TENA

Nsajigwa alisema mastraika Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao walikuwa wameshaanza mazoezi na kikosi cha kwanza, hawatacheza mechi hiyo kwani juzi jioni walijitonesha mazoezini Morogoro. “Tambwe alifanya mazoezi ya siku mbili halafu ameumia tena goti halafu Ngoma yeye amepata maumivu ya misuli tena, hivyo hawatakuwepo kikosini,” alisema Nsajigwa.

Stori na Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge

Comments are closed.