The House of Favourite Newspapers

Yondani Arejea Yanga, Aanza Mazoezi

IKIJIANDAA na mchezo wake wa pili wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, nahodha na beki mkongwe wa Yanga, Kelvin Yondani amekubali yaishe na kurejea kikosini kwa ajili ya mchezo huo.

 

Yanga na Rayon zinatarajiwa kuvaana Mei 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mchezo utakaoanza kupigwa saa moja usiku.

 

Awali, beki huyo ilielezwa aligomea safari ya timu hiyo ilipokwenda kucheza mchezo wake wa kwanza hatua ya makundi dhidi ya USM Algers uliopigwa Algeria kwa Yanga kufungwa mabao 4-0 kutokana mkataba wake kumalizika mwezi uliopita na kudai mshahara wa miezi mitatu.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Kocha Mkuu wa timu hiyo raia wa DR Congo Kinshasa, Zahera Mwinyi alisema beki huyo ameripoti katika mazoezi ya jana Ijumaa yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar, saa kumi kamili jioni.

 

Zahera alisema, anafurahia kurejea kwa beki huyo na baadhi ya wachezaji ambao baadhi bado wamegomea mazoezi yaliyofanyika kwa siku tatu mfululizo kwa kudai mishahara yao ya miezi tatu.

 

Aliwataja wachezaji walioshindwa kuripoti tangu timu hiyo ilipoanza mazoezi wiki hii ni Ibrahim Ajibu na Papy Tshishimbi ambaye yeye anasumbuliwa na majeraha ya enka aliyoyapata mechi na Wollaita Dicha ya nchini Ethiopia katika Kombe la Shirikisho Afrika.

 

“Nimefurahi kumuona Yondani akirejea uwanjani na kuanza mazoezi ya pamoja na wenzake baada ya kukosekana kwa siku hizi mbili, licha ya wengine baadhi kushindwa kutokea.

 

“Kama kocha najaribu kuongea vizuri na wachezaji ili waweze kuripoti tuendelee kujiandaa na mechi dhidi ya Rayon ambayo tutacheza hapa nyumbani ni muhimu kupata matokeo mazuri baada ya kupoteza mchezo uliopita.

 

“Wachezaji wote waliobaki wameripoti mazoezi ya leo (jana) isipokuwa wawili tu kwa waliobaki hapa Dar ambao ni Ajibu na Tshishimbi,” alisema Zahera.

 

Wakati huohuo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema Yondani ambaye alimtemea mate beki wa Simba, Asante Kwasi, alishindwa kutokea kwenye Kamati ya Nidhamu kujibu tuhuma hizo na sasa shirikisho hilo limesema atatumiwa wito wa kuitwa kwa mara nyingine kwenye Kamati ya Nidhamu na asipotokea kesi itasikilizwa upande mmoja.

Comments are closed.