The House of Favourite Newspapers

Dar Yote Nyekundu Leo, Magufuli Kuwakabidhi Kombe Simba

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye ni Simba wa kutupwa, amewaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi leo pale Uwanja wa Taifa kumshuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli akiwakabidhi kombe la ubingwa Simba.

 

Simba imetwaa ubingwa wake kwa mara ya 19 tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo na itakabidhiwa kombe hilo leo Jumamosi katika mchezo wao wa ligi dhidi ya Kagera Sugar utakaoanza Saa 8:15 mchana.

 

“Naomba wapenzi wa soka wajitokeze kwa wingi kuja kushuhudia rais wetu Magufuli akiwakabidhi Simba kombe, inaweza kuwa ni siku ya mapinduzi katika masuala ya soka kutokana na uwepo wake anaweza kutusaidia katika changamoto.

“Pia suala la usalama TFF wameliimarisha hivyo watu wasiwe na hofu na niwapongeze Simba kwa kuleta heshima kubakiza kombe hapa Dar es Salaam ambao ni mkoa ninaousimamia.

 

“Najua Simba haitatuangusha mbele ya rais kufungwa na Kagera naamini kina Okwi (Emmanuel, kinara wa mabao ligi kuu akiwa nayo 20) watatupa heshima tu mashabiki waje kwa wingi wawe wa Yanga, Mbao na wengine wote.

 

“Nitahakikisha matrafiki watakaokuwa zamu wawe makini kuepusha misongamano barabarani ili watu watakapotoka Taifa wawahi nyumbani kufuturu,”alisisitiza Makonda.

 

Salim Abdallah “Try again’ ambaye ni Kaimu Rais wa Simba, alisema: “Tunashukuru kitendo cha rais wa nchi kukubali kuja kuikabidhi Simba kombe siyo jambo dogo zaidi tunaomba wapenzi wa soka wajitokeze kwa wingi kuweza kujaza uwanja bila kujali itikadi zetu.”

 

Haji Manara, Ofisa Habari wa Simba, alisema: “Malengo yetu mpaka sasa ni kumaliza ligi bila kufungwa na tumekubaliana na Bodi ya Ligi kupunguza viingilio vya uwanjani viti vya mzunguko (Orange) Sh 2,000, VIP B Sh 10,000 na VIP A Sh 15,000 ili kuwapa watu wote fursa ya kuingia uwanjani.”

Comments are closed.