The House of Favourite Newspapers

Mzuka Wa Mechi Ya Watani Waanza Yanga

Kikosi cha timu ya Yanga.

YANGA ambayo imepoteza pointi saba mikoani katika mechi tatu mfululizo, leo Jumapili jioni inacheza na JKT Tanzania yenye pointi 32 jijini hapa.

 

Katika mechi tatu zilizopita Yanga ilipoteza moja dhidi ya Stand, ikadroo na Coastal Union na Singida United na kufikisha pointi 55 kileleni mwa msimamo wa Ligi.

 

Kocha wa Yanga,Mwinyi Zahera amesisitiza kwamba wachezaji wake wamejiandaa kisaikolojia kushinda mechi hiyo ili kujiweka sawa na mzuka wa mechi ijayo dhidi ya Simba Februari 16. Baada ya mechi ya leo Yanga itapitiliza Morogoro kujiandaa na mechi ya watani.

JKT Tanzania katika michezo yake 25, imeshinda mechi saba, imepoteza saba na kudroo 11. Katika mechi ya mwisho na Yanga walifungwa mabao matatu rahisi kwenye Uwanja wa Taifa na kusababisha minong’ono juu ya kiwango cha JKT.

 

Takwimu za mchezo huo zinaonyesha kwamba timu zote zilipiga mashuti sita ya maana langoni, huku Yanga ikicheza faulo 19 dhidi ya 16 za Wanajeshi hao wa Mbweni, Dar es Salaam.

 

Lakini rekodi yao ya kuvutia kabla ya kuwavaa Yanga leo ni kwamba, wamefunga mabao 15 na wameruhusu idadi hiyohiyo tangu msimu huu uanze.

 

Katika mchezo wa leo, Bakari Shime wa JKT amesisitiza watacheza aina ya mchezo wao, miongoni mwa mastaa atakaowategemea ni Mwinyi Kazimoto, Azizi Gilla, Frank Nchimbi na Abrahaman Mussa.

 

Simba watakuwa kwenye runinga zao jioni wakiangalia mechi hiyo pekee, huku wakijiandaa na mchezo wao wa marudiano na Al Ahly Jumanne Jijini Dar es Salaam.

Comments are closed.