The House of Favourite Newspapers

Kesi Ya Wambura Bado Ngoma Nzito

 

Michael Wambura.

IMEELEZWA kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kufuta wala kusikiliza kesi ambayo inamkabili aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura.

 

Hatua hiyo imewekwa wazi kutokana na utata ambao ulijitokeza katika hati ya mashitaki ambayo ilitoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) huku wakili wa mshitakiwa, Majula Magafu akidai kuwa hati ya mashitaka ilionyesha kuwa ni kesi ya jinai lakini baadaye ilibadilishwa kwa mkono na kuwa kesi ya uhujumu uchumi ambapo amedai kuwa makosa ya mshitakiwa hakuna hata moja la uhujumu uchumi.

 

Wambura ameshitakiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) huku akikabiliwa na mashitaka 17 na kati ya hayo mashitaka mawili ya kutakatisha fedha na lingine likiwa la kughushi nyaraka.

 

Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina amesema amepitia hoja za pande zote na anatupilia mbali mapingamizi ya upande wa utetezi.

Akifafanua sababu za kutupilia mbali alisema pamoja na kifungu hicho cha 129 cha CPA, kifungu cha 3 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, kinaondoa mamlaka kwa Mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi, isipokuwa DPP atakapowasilisha kibali cha kuiruhusu mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.

 

Mhina aliiambia mahakama kuwa mashauri hayo ya pande zote mbili wa serikali na mshitakiwa yaliweza kufanyiwa kazi na mahakama na kubaini haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, wala kutoa dhamana kwa mshitakiwa na pia mshitakiwa hana uwezo wa kukata rufaa.

 

Alieleza kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya kumsomea mashitaka mtuhumiwa huyo, suala la kubadili hati ya mashitaka litajadiliwa katika mahakama ambayo kesi hiyo itapelekwa.

 

Hata hivyo, wakili wa Wambura, Emmanuel Muga aliwasilisha ombi lake kwa mahakama kwa kutaka kufahamu ni vifungu gani ambavyo walitumia Takukuru na wao binafsi kumkamata mteja wake, lakini hakupata majibu na badala yake ikaelezwa kuwa itafafanuliwa Februari 28, mwaka huu ambapo kesi hiyo itatajwa tena.

 

Comments are closed.