The House of Favourite Newspapers

SENEGAL YATINGA FAINALI BAADA YA MIAKA 17 -VIDEO

PATASHIKA nguo kuchanika ilitokea jana katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali kati ya Senegal na Tunisia kwenye Uwanja wa 30 June jijini Cairo na Senegal wakafanikiwa kutinga fainali kwa ushindi wa bao 1-0.

 

Bao hilo muhimu lilipatikana dakika ya 100, ikiwa ni ndani ya dakika 30 za nyongeza, likifungwa na beki wa Gent ya Ubelgiji, Dylan Bronn aliyejifunga.

 

Awali, dakika 90 za mchezo huo zilimalizika kwa suluhu lakini ulikuwa ni mchezo wenye mvuto wa aina yake huku kila timu ikitengeneza mashambulizi ya kuvutia lakini hakuna iliyopata bao.

Mfano, dakika ya 25, Youssef Sabaly wa Senegal ambaye anakipiga Boudreaux ya Ufaransa, aligongesha mwamba wakati Senegal wakilisakama lango la wapinzani wao kama nyuki kwa dakika 25 za kwanza.

 

Sadio Mane alibaki yeye na lango dakika ya 36 lakini akapiga nje, dakika ya 56 Mane pia alibaki na kipa ambaye aliudaka mpira wakati staa huyo wa Liverpool akijaribu kumzunguka Tunisia nao hawakuwa nyuma.

 

Timu hizo zilikuwa zikishambuliana kwa zamu. Dakika ya 64, staa wa Esperance, Mtunisia Yassine Khenissi alishindwa kufunga akiwa amebaki na kipa. Kivutio kikubwa ilikuwa ni dakika ya 73 ambapo Tunisia walipata penalti lakini kiungo wa Zamalek, Ferjani Sassi akakosa.

 

Beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly aliunawa mpira ndani ya eneo la hatari, akapewa kadi ya njano, hivyo atakosa fainali kwa kuwa hiyo ilikuwa kadi yake ya pili ya njano ya michuano hiyo.

 

Lakini dakika sita baadaye, Senegal nao walipata penalti ambayo kiungo wa Newcastle, Henri Saivet alikwenda kupiga na kukosa! Huu ulikuwa ni mtanange kati ya timu inayoshika namba moja kwa ubora Afrika, Senegal, na ile inayoshika namba mbili kwa ubora barani humo, Tunisia.

 

Senegal hawajawahi kutwaa Afcon na hii ni fainali yao ya pili, awali walitinga fainali mwaka 2002 wakati kocha wao wa sasa Alliou Cisse ‘Rasta’ akikipiga kama kiungo mkabaji, sasa imepita miaka 17 ndio wanatinga fainali ya pili. Zikiwa zimebaki dakika 9 kabla ya dakika 30 za nyongeza kumalizika, Tunisia walidhani wamepata penalti baada ya mwamuzi kutenga lakini waliporejea kwenye VAR, mwamuzi akabadili mawazo.

 

Tunisia wamepoteza nafasi ya kutwaa ubingwa wa Afcon kwa mara ya pili. Fainali itachezwa Ijumaa kati ya Senegal na mshindi wa mechi ya jana usiku kati ya Nigeria na Algeria.

Comments are closed.