The House of Favourite Newspapers

LICHA YA KISUKARI, PRESHA… UGONJWA MPYA WA CHOKI WASHITUA

DAR ES SALAAM: WAKATI bado akiwa kitandani akisumbuliwa na maradhi ya presha na kisukari, ugonjwa mpya wa staa wa muziki wa Dansi, Ali Choki ameeleza kusumbuliwa na ugonjwa mpya ambao unashtua, Amani linakupa habari kamili.  

 

Awali, ilifahamika kuwa Choki anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na presha ambapo alilazwa katika Hospitali ya Bugando, Mwanza ambako alikuwa hoi mpaka kufikia hatua ya kulazwa katika chumba cha uangalizi maalum ‘ICU’ na kuwekewa mashine ya kupumulia ‘oxygen’.

 

HUYU HAPA CHOKI

Akizungumza na Amani kwa shida huku sauti yake ikiwa kwa mbali kwa njia ya simu siku chache baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali, Choki alisema bado anaumwa na yupo Mwanza bado kwani madaktari wamemtaka atumie dawa kwa wiki mbili ndipo waangalie kama anaweza kwenda Dar au laa.

 

UGONJWA MPYA

Aliendelea kueleza kuwa tofauti na magonjwa ya awali ya presha na kisukari, madaktari pia waligundua kuwa mapafu yamejaa maji hivyo wakampa dozi ya dawa za wiki mbili kwa ajili ya kuyakausha.

“Licha ya kwamba nimeruhusiwa kutoka hospitali lakini bado niko kitandani naendelea na dawa nilizopewa za wiki mbili na baada ya hapo niliambiwa nirudi kwa ajili ya kuangalia kama maji yameisha kwenye mapafu ndipo niweze kurudi Dar kwanza. “Nashukuru madaktari walisema kwamba waliyawahi maji hayo ndiyo maana wamenipa dawa  za kukausha lakini ingekuwa vinginevyo yangekuwa hatari zaidi,” alisema Choki.

 

AWAOMBA WATANZANIA WAMUOMBEE

Akizidi kuzungumza na Amani kuhusu afya yake, Choki aliwaomba Watanzania wamuombee dua kwani hali yake bado haijatengemaa. “Bado naumwa sijawa sawa nina nafuu kiasi tu hivyo ninawaomba Watanzania na mashabiki wangu waniombee dua kwa Mwenyezi Mungu ili nipone niweze kurudi kwenye muziki kama zamani niweze kuwaburudisha,” alisema Choki.

 

UGONJWA WASHTUA

Baada ya kugundulika kwa ugonjwa huo mpya watu wengi wa karibu wakiwemo ndugu wa Choki walijikuta wakishtuka kwani hawakutegemea kama kuna ugonjwa zaidi ya

presha na kisukari uliokuwa unamsumbua awali. “Dah! Kiukweli tumuombee sana Choki maana huu ugonjwa wa mapafu kujaa maji ni hatari na ndiyo maana alizidiwa sana mpaka kufikia hatua ya kupumulia mashine ‘oxygen’, bado hali yake haijawa ya kuridhisha anaendelea na matibabu nyumbani,” alisema mmoja wa marafiki wa karibu wa Choki ambaye hakutaka jina lake litajwe.Image result for ALICHOKI

NINI SABABU YA MAPAFU KUJAA MAJI?

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na ugonjwa huo, Dokta Godfrey Chale ‘Dk. Chale’ alieleza kuwa ugonjwa huo husababishwa na bakteria ambapo mgonjwa hushindwa kupumua vizuri, maumivu ya kifua, kifua kikuu na vichomi. Dk. Chale alieleza kuwa endapo mgonjwa atatibiwa vizuri atapona lakini asipopata matibabu mazuri haponi kwa dawa tu itabidi atobolewe maji yatolewe kwenye mapafu.

 

TUJIKUMBUSHE

Choki mkongwe wa dansi nchini, kabla ya kukumbwa na maradhi hayo, alikuwa akiitumikia Bendi ya Super Kamanyola ya jijini Mwanza akitokea Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’.

Choki amejiunga na kutoka Twanga kwa nyakati tofauti. Aliwahi pia kutamba na bendi yake ya Extra Bongo ambayo ilidumu kwa kipindi fulani na kuleta ushindani kwa Twanga lakini baadaye ilikufa. Ilipokufa ndipo Choki aliporejea Twanga kwa mara ya nyingine kabla ya kutimkia Super Kamanyola.

Miongoni mwa vibao vikali vya Choki ambavyo vinatikisa kwenye ulimwengu wa dansi ni pamoja na Sisi ndio Sisi aliomshirikisha marehemu Banza Stone.

Comments are closed.