The House of Favourite Newspapers

Maisha Ya Ray C Na Kilichompata, Mdogo Wangu

Mwanamuziki Rehema Chalamila ‘Ray C’.

MWAKA 2012, tarehe siikumbuki vizuri, nikiwa katika ofisi zetu za zamani maeneo ya Bamaga, Mwenge jijini Dar, nilipigiwa simu na dada wa mapokezi akiniambia kwamba, kuna kijana amefika hapo na kudai ana habari nzito kuhusu staa mkubwa sana!

Niliposikia hivyo, kwa kuwa nilikuwa na kiu ya habari, nilinyanyuka na kwenda kumuona ‘sosi’ huyo.

Kwa wasiojua, sosi ni mtu ambaye siyo mwandishi lakini analeta habari au anatoa taarifa kuhusu tukio ambalo amelipata huko mtaani.

 

Basi, nilipofika mapokezi, nikakutana na kijana mmoja akiwa anachezea simu yake. Baada ya kuniona, akaniambia ana habari inayomhusu mwanamuziki Rehema Chalamila ‘Ray C’.

Akafungua simu yake na kunionyesha picha za Ray C akiwa amezima ndani ya Bajaj baada ya kutumia madawa ya kulevya. Sikuamini kama yule ni Ray C, nilimkatalia katakata kuwa, hakuwa Ray C yule niliyemfahamu.

Hapo ni baada ya kuwepo kwa tetesi za muda mrefu kuwa, mwanadada huyo alikuwa akitumia madawa ya kulevya.

Baada ya kuzichunguza sana zile picha, hatimaye nilithibitisha kwamba alikuwa ni Ray C ‘Kiuno Bila Mfupa’. Niseme ukweli kwamba, siku hiyo machozi yalinitoka! Niliumia kupita maelezo.

 

Kilichonifanya nisikie uchungu ni kwamba, Ray C alikuwa ni kati ya wasanii ambao nilikuwa nawakubali. Staili yake ya uimbaji, uchezaji wake na hata muonekano wake vilinifanya nimpende.

Lakini baada ya kuona picha zake, nikajisemea kwamba, Ray C ndiyo basi tena! Niliamini kifo kilikuwa karibu yake.

Mimi kama mwandishi, kuna wakati ubinadamu uliniingia, nikatamani ninunue zile picha kisha nisiiandike ila habari lakini nikaamua tu kuandika ili jamii ijue yuko kwenye hali gani na iweze kumsaidia.

 

Baada ya habari hiyo kutoka, nchi ilitikisika! Hali mbaya ya Ray C ikawa ndiyo gumzo na harakati zikaanza za kumsaidia.

Wakati huo hakuwa na mbele wala nyuma, kauza kila kilichokuwa chake, unajua tena ukishakuwa teja!

Kwa nini nimeanza kugusia kidogo kuhusu historia hiyo? Ni kwa sababu nataka leo wewe msomaji wangu, utumie kile kilichompata Ray C miaka ile na hali aliyonayo sasa hivi kuamini kwamba Mungu yupo na hutakiwi kukata tamaa!

 

Asilimia kubwa ya watu waliomuona Ray C kipindi kile waliamini kwamba asingepona, wengi walishamkatia tamaa. Lakini kuonesha kwamba, Mungu yupo na yeye ndiye anayepanga kila jambo, Ray C wa leo ni mpya kabisa. Anawaka, amenenepa na amenawiri. Ukiutembelea ukurasa wake wa Instagram utaona anatupia mapichapicha akiwa nchini Uingereza, anakula bata, yaani siyo Ray C yule ambaye watu walishamuona ni marehemu anayetembea.

 

Sasa, tuna lipi la kujifunza kwa mwanadada huyu? Huenda yapo mengi lakini mimi nitazungumzia mawili tu. Kwanza, historia ya maisha ya Ray C itupe fundisho kwamba, Mungu akiwa bado anakuhitaji uendelee kuishi, hata kama uko kwenye hali mbaya kiasi gani, bado anaweza kukurudisha kwenye hali nzuri.

 

Yeye anaamua tu kwamba, flani nimuingize kwenye majaribu haya ili iwe fundisho kwa wengine.

Lakini kingine ambacho tunaweza kujifunza kwa Ray C ni kwamba, kama tuliwahi kuteleza, tukafanya mambo ambayo hayafai na hatimaye kuingia kwenye majanga, tukiamua kubadilika, tunaweza kurudi kwenye maisha yetu mazuri.

 

Ray C kweli alihadaika, akajiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya, achungulia kifo lakini baadaye alipogundua kwamba hayuko salama na usalama wake ni kubadilika, Mungu alimsimamia na sasa ndiye huyu tunayemuona.

Kuna watu wengi sana huko mtaani ambao wako kwenye hali aliyokuwa nayo Ray C miaka ile, wanaona maisha hayana thamani tena kwao, eti wanasubiri tu kifo kiwachukue, hapana! Tulio karibu nao tuwasaidie wajitambue na wabadilike na kuwaaminisha kwamba bado wana nafasi nyingine ya kuishi maisha mazuri.

 

Mfano mzuri ni mimi. Katika familia yetu tuna mdogo wetu ambaye alikuwa anapita kwenye njia alizopita Ray C. Mdogo wetu huyu amekuwa mtumiaji mzuri sana wa pombe na kuvuta bangi.

Maisha yake yaliharibika kuliko neno lenyewe, kila akipata pesa yeye ni pombe tu. Jamii ilishaanza kumchoka, kuna hata ndugu walishamkatia tamaa lakini baadhi yetu tukasema hapana!

 

Tulidhamiria kumbadilisha, tulitumia kila mbinu kuhakikisha tunamuokoa kwenye dimbwi la ulevi na uvutaji bangi.

Bahati nzuri sana Mungu ametusimamia na leo ni kijana mzuri ambaye anayaendesha maisha yake kwa kufanya biashara.

 

Ushauri wangu ni kwamba, tutumie historia ya Ray C kuwasaidia wale ambao wako kwenye wakati mgumu.

Tusiwakatie tamaa, naamini hata Ray C asingepewa msaada unaostahili, leo hii tungekuwa tunaongea mangine.

Comments are closed.