The House of Favourite Newspapers

Barnaba Anakijiji cha Watoto wa Kike

0

UKIZUNGUMZIA wanamuziki wazuri Bongo hii wanaojua kuimba, kutunga, kutumia vyombo na kuzalisha (produce) ngoma kali za Bongo Fleva, huwezi kuacha kumtaja Elias Barnabas, muite Barnaba Boy ‘Classic’. Barnaba ni zao la Tanzania House of Talent (THT). Mwenyewe anasema ana miaka 17 kwenye gemu la Bongo Fleva. Katika mahojiano maalum na Over Ze Weekend, Barnaba anafunguka mengi;

Over Ze Weekend: Mashabiki wako mara nyingi wanasema huwa wanashindwa kujua wewe ni mtu wa dizaini gani? Barnaba: Ni mtu kama watu wengine ila tofauti yangu mimi ni msanii. Pia ni mtu ambaye napenda amani, napenda watu na kingine mimi napenda kukosolewa pale ninapokosea. Bila kusahau napenda sana kumcha Mungu na kufanya kazi kwa bidii.

Over Ze Weekend: Mashabiki wanajua una kipaji kikubwa cha muziki, ni nani alikigundua? Barnaba: Ni mama mzazi.

Lakini baada ya hapo nilikwenda THT ambapo nilipokelewa na marehemu Ruge. Ni mtu ambaye alinipokea na kunilea nikiwa mdogo. Alinisainisha THT kisha nikaanza masomo ya muziki.

Over Ze Weekend: THT ina mchango gani kwenye muziki wako? Barnaba: Mchango wake hauelezeki wala hauhesabiki maana safari yangu ya muziki ilianzia pale. Nilifika pale nikiwa sijui kitu kuhusiana na muziki, nilianza kusoma, kuandika nyimbo kisha nilijifunza kucheza na vyombo vya muziki.

Over Ze Weekend: Ni wimbo gani uliokutambulisha kwenye gemu na kukufanya ukajulikana Barnaba ni nani? Barnaba: Njia Panda ni wimbo ulionitambulisha rasmi kwenye muziki ambao niliimba na msanii Pipi. Pia ndiyo wimbo uliobeba album yangu ya kwanza ya Njia Panda.

Over Ze Weekend: Mpaka sasa una jumla ya album ngapi? Barnaba: Nina albam nne ambazo ni Njia Panda, Barnaba One, Gold na Kichwa Changu. Over Ze Weekend: Ngoma ya Mapenzi Jeneza ni kisa cha kweli au? Barnaba: Kila kitu ninachoimba, ninakiimba kwa sababu ya matukio

ninayoyaona. Siimbi kwa sababu ya mtu. Mimi ni mfanyabiashara, hivyo ninafanya ubunifu kupata ladha nzuri kwenye muziki wangu. Stori kwamba ni kisa kinachonihusu, si kweli.

Over Ze Weekend: Wewe ni mtunzi mzuri, je, ni wasanii gani uliwahi kuwatungia ngoma na ‘zika-hit’? Barnaba: Ni wengi sana. Nina kijiji changu cha wasanii wa kike kama Linah, Vanessa, Mwasiti, Ruby, Recho, Lulu Diva, Shilole na wengine wengi.

Over Ze Weekend: Hujajibu swali la ni ngoma gani umemuandikia msanii na ikafanya vizuri mno? Barnaba: Nimeandika ngoma nyingi sana ambazo zimefanya vizuri na zimewatoa wasanii kama vile Siyo Kisa Pombe ya Mwasiti, Na Yule ya Ruby, Hamjui ya Vanessa na nyingine nyingi. Mbali na kuwasaidia, pia ninalipwa. Utunzi umekuwa ni biashara kubwa kwangu, japokuwa mwanzoni nilianza bila kulipwa, lakini baadaye nikawa nalipwa. Ninafurahi kuwa daraja la wasanii wengi.

Over Ze Weekend: Una kipaji cha kupiga gitaa, je, ulizaliwa nacho au ulijifunza? Barnaba: Ofcourse nilizaliwa nacho, lakini baadaye nilikwenda kujifunza. Nilipofika THT nilijifunza zaidi kupiga gitaa.

Over Ze Weekend: Ulishawahi kushinda tuzo yoyote nje ya nchi? Barnaba: Mbali na tuzo za hapa nyumbani pia  nimeshashiriki na kushinda Tuzo ya Best Male Vocalist ambayo niliipata Marekani.

Over Ze Weekend: Una kolabo yoyote na msanii wa nje ya nchi?

Barnaba: Zipo nyingi tu. Nimefanya ngoma na Nyota Ndogo na Sauti Sol wa Kenya na Jose Chameleone wa Uganda.

Over Ze Weekend: Ni msanii gani Bongo ambaye unakubali kazi zake na unatamani kufanya kolabo naye?

BARNABA: Kwa upande wangu hakuna ambaye ninamtamani, yeyote atakayejitokeza nipo tayari kufanya naye kazi.

Over Ze Weekend: Kwa wasanii wa kike unamkubali nani? Barnaba: Ninawakubali wote ila kwa wasanii ninaowapenda zaidi hapa Tanzania ni Vanessa na Jide.

Over Ze Weekend: Vipi kuhusu usimamizi? Au unajisimamia mwenyewe? Barnaba: Mimi ninajitegemea, natuma watu wafanye kazi siyo mimi kusimamiwa na watu kwa sababu mimi ni msanii wa muda mrefu kwenye gemu.

Leave A Reply